Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Martin K. Ngoga ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 26 Januari, 2021.
Viongozi hao wamejadili namna watakavyoimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Bunge hilo la Afrika Mashariki na kuliwezesha Bunge hilo kutekeleza majukumu yake kikamilifu huku likizingatia sheria, kanuni , taratibu na uadilifu.
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Waziri Ole Nasha amemtaarifu Spika huyo wa Bunge la Afrika Mashariki kwamba Tanzania imekua ikifanya juhudi kubwa katika kuhakikisha nchi za Afrika ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaimarisha mtangamano na kuongeza kwamba Bunge hilo la Afrika Mashariki ni moja kati ya vyombo muhimu sana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki vinavyoimarisha mtangamano.
Amemuomba Mhe. Spika kuendelea kulisimamia Bunge hilo kwa kufuata Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, Itifaki na Kanuni za Jumuiya ili kuzingatia utawala bora.
Naibu Waziri amemkumbusha Spika huyo kwamba Bunge la Afrika Mashariki ni chombo kinachoziangalia taasisi za Jumuiya hivyo lazima kiwe chombo cha mfano kwa Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika uendeshaji wa shughuli zake na kuzingatia weledi.
Akizungumzia kuhusu bajeti ya Jumuiya kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Mhe. Naibu Waziri alimtakia heri katika kupitisha Bajeti hiyo kwenye Mkutano wa Bunge hilo utakaofanyika mwanzoni mwa mwezi Februari, 2021.
Naye Mhe. Spika Ngoga ameshukuru kwa maoni na msimamo wa Tanzania katika masuala mbalimbali ndani ya Jumuiya na kuelezea masikitiko yake baada ya Bunge kushindwa kupitisha Bajeti iliyowasilishwa na Baraza la Mawaziri la Jumuiya.
Ameahidi kuyafanyia kazi maoni ambayo ameyapokea kutoka kwa nchi wanachama ikiwamo Tanzania kwa ajili ya manufaa ya nchi hizo na wananchi wake na kuongeza kuwa atatumia uzoefu wake kuhakikisha Bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inapitishwa na Bunge ili shughuli za Jumuiya ziendelee.