NAIBU WAZIRI UMMY ATAKA MASUALA YA WATU WENYE ULEMAVU KUJUMUISHWA NA KUJADILIWA KWENYE MABARAZA YA MKOA NA WILAYA

Sehemu ya Viongozi wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Mkoa wa Tabora na watendaji katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakisikiliza kwa makini maelezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika mkoa huo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kujumuisha na kuweka ajenda za masuala ya wenye ulemavu kwenye Mabaraza ya mashauriano ya Mkoa (Regional Consultative Councils) na Mabaraza ya Mashauriano ya Wilaya (District Consultative Councils) ili kuweza kuhakikishia watu wenye ulemavu wanapata huduma bora, haki na ustawi katika jamii zinazowazunguka.

Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo Mkoani Tabora alipokutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi wa Mkoa huo pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) katika Mkoa huo, Mheshimiwa Ummy alibainisha kuwa masuala ya Watu wenye ulemavu yakijumuishwa kwenye mabaraza ya mashauriano ya Mkoa aua Wilaya itasaidia kuibua mikakati ya ujumuishaji, usimamizi na utekelezaji wa masuala ya wenye Ulemavu nchini.

Ad
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Philemon Sengati (kushoto) akieleza jambo kuhusu namna mkoa huo ulivyojipanga katika kuhudumia masuala ya Watu wenye Ulemavu na kuzuia vitendo vya Usafirishwaji na Utumikishwaji wa watu wenye ulemavu kuombaomba mitaani. (Katikati) ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu Ndg. Jacob Mwinula (kulia).

“Katika kuhakikisha kuwa mipango mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu inapatiwa ufumbuzi ni bora wakati wa vikao vya mabaraza ya Mashaurianao ya Mkoa na Wilaya mkajumuisha masuala kundi hilo maalum, kwa kufanya hivyo itawawezesha kutambua mahitaji yao ya msingi na hamtawaacha nyuma watu wenye ulemavu katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo,” alieleza Ummy

Aliongeza kuwa, bajeti zinapoandaliwa pia kuanzia ngazi ya Mkoa zijumuishe masuala ya watu wenye ulemavu ili kuhakikisha mipango ya kundi hilo ya kimaendeleo inatiliwa mkazo kwa lengo la kuinua kiwango cha utoaji huduma kwa kundi hilo.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Tabora Bw. Panin Kerika (aliyesimama kulia) akitoa taarifa fupi ya mkoa kuhusu ushughulikiwaji, ufuatiliaji na uhamasishaji wa masuala ya kisera, kisheria na miongozo kuhusu huduma kwa watu wenye ulemavu kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga wakati wa ziara yake ya kikazi katika mkoa huo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Tabora pamoja na pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Mkoa huo alipofanya ziara ya kikazi iliyolenga kupokea taarifa ya ushughulikiwaji, ufuatiliaji na uhamasishaji wa masuala ya kisera, kisheria na miongozo kuhusu huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kuwafikia wenye ulemavu vijijini. (Watano kutoka kushoto) ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Philemon Sengati.

Alifafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa ikiwajali watu wenye ulemavu sambamba kuboresha huduma zao za msingi ikiwemooo afya, elimu, miundombinu n.k, huku akielezea pia juu ya namna uzingatiwaji huo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Ibara ya 94, 95 na 96 ambazo zinaelezea na kufafanua mwelekeo wa namna masuala ya  Watu wenye Ulemavu yatakavyokuwa yakishughulikiwa, kuendelea kutambua na kuwapatia kipaumbele katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Sambamba na hayo, Naibu Waziri Ummy alihimiza juu ya kuimarishwa kwa huduma za afya na zenye staha kwa watu wenye ulemavu ikiwemo upatikanaji wa mafuta kwa wale wenye ulemavu wa ngozi (Ualbino), kuimarisha ulinzi, kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi, kuwapatia elimu kwa kuimarisha elimu jumuishi, kujengwa kwa miundombinu fikivu na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na masuala mbalimbali ya wenye ulemavu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega wakati wa Ziara yake ya kikazi iliyolenga kupokea taarifa ya ushughulikiwaji, ufuatiliaji na uhamasishaji wa masuala ya kisera, kisheria na miongozo kuhusu huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kuwafikia wenye ulemavu vijijini.

Aidha, Mheshimiwa Ummy amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwa walezi wa watu wenye ulemavu waliopo kwenye maeneo yao ili kujenga ushirikiano Naibu Waziri aliwataka Wakuu wa Miko ana Wakuu wa Wilaya kuwa karibu na kuwa walezi wa watu wenye ulemavu waliopo katika maeneo yao ili kuwawezesha kujadili mambo mbalimbali yanayohusu kundi hilo maalum. Pia ametaka mabaraza ya Watu wenye Ulemavu yaliyopo kuwa hai ili yaweze kujadili namna bora ya kuhudumiwa kundi hilo.

Aidha, Mheshimiwa Ummy alitumia fursa hiyo kukemea vitendo vya usafirishwaji na utumikishwaji watu wenye ulemavu kuombaomba mitaani na badala yake amewasihi watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ya asilimia 2% ili waanzishe miradi mbalimbali ya kiuchumi.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu Ndg. Jacob Mwinula akieleza jambo wakati wa kikao cha upokeaji wa taarifa kilichoongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.

“Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa mikoa kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu watu wenye ulemavu waliopo kwenye maeneo yenu kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, halmashauri, kata hadi vijijini ili kuzuia vitendo vya usafirishaji na utumikishwaji wa watu wenye ulemavu kuombaomba mitaani,” alisisitiza

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Philemon Sengati alisema kuwa Mkoa wa Tabora umekuwa stari wa mbele katika kuhudumia watu wenye ulemavu, huku akitolea mfano namna uongozi wa mkoa huo umekuwa ukishirikiana na viongozi kwa watu wenye ulemavu katika kushughulikia kwa pamoja masuala mbalimbali ya kundi hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mhe. John Mwaipopo akifafanua jambo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga kuhusu wilaya hiyo inavyoshughulikia masuala mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu.

Pia, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliahidi kuwa mkoa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, mamlaka za serikali za mitaa watahakikisha watu wasio waadilifu katika jamii na wenye nia ovu katika kuwatumia watu wenye ulemavu wanachukuliwa hatua.

“Mkoa wa Tabora utaendelea kutoa huduma bora kwa Watu wenye Ulemavu kama sehemu ya utekelezaji wa mikataba na miongozo iliyopo katika kushughulikia masuala ya kundi hilo,” alisema Sengati

Mwenyekiti wa Chama Cha Wasioona Mji wa Nzega akitoa shukrani kwa Serikali namna ambavyo imekuwa ikiwajali Watu wenye Ulemavu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu Ndg. Jacob Mwinula alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushughulikia na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu nchini sambamba na kuhakikisha kundi hilo linapata huduma bora.

Katika Ziara hiyo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Halmashauri ya Mji wa Nzega, Halmashauri ya Wilaya ya Igunga lengo ikiwa kupokea taarifa ya ushughulikiwaji, ufuatiliaji na uhamasishaji wa masuala ya kisera, kisheria na miongozo kuhusu huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kuwafikia wenye ulemavu vijijini.

Pia, Naibu Waziri alitembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma za Marekebisho kwa Watu wenye ulemavu Ruanzali kilichopo Mkoani Tabora.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *