Waziri Kilimo Prof Adolf Mkenda leo ameanza ziara ya kikazi wilayani Mvomero kwa lengo la kukagua miradi ya umwagiliaji na hali ya uzalishaji sukari kwenye kiwanda cha Mtibwa pamoja na kuongea na wakulima.
Awali akongea na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero Prof.Mkenda amewataka waendelee kusimamia kazi za kilimo ikiwemo miradi ya umwagiliaji ili wakulima waongeze tija na kuweza kulima zaidi ya mara moja kutokana na wilaya hiyo kuwa na maeneo mazuri kwa umwagiliaji.
Prof. Mkenda alisema wizara yake inapitia upya utendaji kazi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ikiwemo kutafuta watumishi wenye weledi wa kubuni na kusimamia miradi yenye kutoa tija kwa wakulima.
” Suala la umwagiliaji bado lina shida,tunahitaji kulipatia suluhu ya mapema kwani haiwezekani serikali ijenge miundombinu halafu uzalishaji uwe na tija ndogo na wakati mwingine wakulima washindwe kutunza miundombinu kama kulipia umeme” alisema Prof. Mkenda
Akizungumza kuhusu sekta ya sukari Waziri Mkenda alisema tayari mkakati wa kuona uzalishaji sukari unaongezeka umeanza kwa kuwataka wawekezaji kutumia fursa ya kilimo cha umwagiliaji kukuza tija na kutumia mbegu bora za miwa.
Aliongeza kusema serikali itaendelea kuweka mazingira sawa ili kuwe na ushindani sawa kwa wawekezaji na nchi izalishe sukari nyingi.
“Nahimiza uwekezaji katika sekta ya sukari na kuwa serikali itasimamia ushindani ili nchi iwe na uhakika wa uzalishaji na hivyo wawekezaji zaidi wanakaribishwa nchini” alisisitiza Mkenda.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya alisema wilaya ina eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hekta 77,005 kati yake hekta 30,802 zinalimwa na kuomba wizara ya kilimo isaidie uanzishwaji wa miradi mingi ya umwagiliaji.
Mkuu huyo wa wilaya alisema sekta ya kilimo imechangia mapato ya halmashauri kwa asilimia kati ya 25.9 hadi 34 ambapo katika mwaka 2019/20 iliwezesha halmashauri kutoa mikopo ya shilingi milioni 23 kwa vikundi 30 vinavyojishughulisha na kilimo.
Katibu Mkuu Kilimo Gerald Kusaya pamoja na watendaji wakuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB), Bodi ya Sukari na Mrajis Mkuu wanashiriki ziara hiyo pia.