TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA MAENDELEO – RIDHIWANI KIKWETE

Na. Andrew Chale, Chalinze

Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amewashukuru na kuendelea kuwakaribisha Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha sambamba na Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho (IFM) kwa kutenga muda wao na kusaidia jamii ndani ya jimbo hilo.

Ad

Ridhiwani Kikwete ametoa shukrani hiyo, alipokuwa mgeni rasmi wakati wa hafla maalum ya kukabidhi vifaa na vitu mbalimbali kwa Wanafunzi wenye uhitaji maalum (Walemavu) shule ya sekondari Lugoba sambamba na Wananchi wasiojiweza tukio lililofanyika viwanja vya shule Lugoba.

Wanafunzi wenye mahitaji maalum wakisoma Risala yao kwa Mgeni Rasmi.

Awali akitoa neno la shukrani katika hafla hiyo, Ridhiwani Kikwete alipongeza juhudi za wanafunzi hao kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii.

“Nawapongeza sana hii ni mara yenu ya pili kuja kusaidia jamii yenye uhitaji ndani ya Chalinze, leo hii mmefika hapa katika shule hii ya sekondari ya Lugoba ni sehemu sahihi kwani tuna Wanafunzi pia wenye uhitaji maalum wakisoma hapa na wanafanya vizuri sana hivyo misaada hii itaendelea kuwa chachu kwao na pia wanananchi wenye uhitaji.” Alisema Ridhiwani Kikwete.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete akipokea picha ya aliyekuwa Mlezi wa Shule ya Sekondari ya Lugoba marehemu Bwana Shubash toka kwa Binti wa kidato cha kwanza, alipofanya ziara shuleni hapo Februari 21, 2021.

Ridhiwani Kikwete pia alitumia wasaha huo kuwafikishia ujumbe wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwakumbuka wanafunzi wa shule hiyo ambayo aliwahi kusoma. “Niwafikishie ujumbe wa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ambaye alisoma shule hii ya Lugoba, amewashukuru sana na amesema niwafikishie salamu zake hizi kwenu, anawashukuru na anauenzi msaada wenu mliotupatia”. Alisema Ridhiwani.

Wanafunzi hao mbali ya kutoa misaada ya vitu mbalimbali pia walitoa Kadi za Bima ya Afya za CHF kwa Kaya 32 huku Mbunge akiwaunga mkono kwa kulipia Kaya 12.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete akikabidhi chakula kwa Wazee wanaoishi katika mazingira magumu

“Kwa hatua yenu hii ya kulipia Kaya 32 kadi za bima ya afya, Mimi naongeza kaya 12 ambazo nitalipia mimi kuwaunga mkono” Alisema Ridhiwani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wanafunzi, Bwana Michael Boniface ambaye ndiye aliyekuwa anasimamia shughuli hiyo alimshukuru Mbunge kwa kuwapokea na kukubali kuwa mgeni rasmi.

“Sisi kama wanafunzi wa IFM tumeweza kujikusanya na tulichokipata tunaomba mkipokee kwa mikono miwili, mbali ya vitu pia tumechangia damu ambayo tunaamini inakwenda kusaidia wahitaji mbalimbali kwenye hospitali ya Wilaya ya Chalinze pamoja na hilo tumeleta vifaa vya kupimia presha pia” alisema.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete akikabidhi kitambulisho cha Bima ya Afya kwa Mama wa Chalinze

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho (IFMSO), Zubeda Kaduguda aliushukuru uongozi wa chuo cha IFM kwa kuwajengea mazingira mazuri na wao kufanikisha jambo hilo.

“Tunawashukuru sana walezi na wasimamizi wetu na kwa upekee pia niwashukuru Mkuu wa shule ya Sekondari Lugoba, Mbunge na viongozi wote wa Serikali kwa kujumuika nasi siku ya leo”Alisema Rais.

Aidha, aliwahusia Wanafunzi waliojitokeza katika hafla hiyo kuwa na muda mzuri wa kujisomea sambamba na kumtanguliza Mungu mbele kwa kila jambo ili waweze kutimiza ndoto zao.

Hii ni mwaka wa pili kwa Wanafunzi hao wa IFM kusaidia jamii ambapo walifanya hivyo mwaka jana huku mwaka huu wakifanya kwa mara ya pili wakiwa na kauli mbiu ”Charity brings life again to those who are spiritual dead”

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *