RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA KIWANDA CHA USHONAJI BOHARI KUU YA JESHI LA POLISI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi pamoja na Wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi Ujenzi wa Kiwanda cha ushonaji Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi na kufungua Ofisi, Madarasa na Mabweni ya Chuo cha Taaluma cha Polisi Kurasini mkoani Dar es Salaam leo tarehe 26 Februari 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli tarehe 26 Februari, 2021 ameweka jiwe la msingi la kiwanda cha ushonaji bohari kuu ya Jeshi la Polisi na amefungua majengo ya ofisi, madarasa na bweni la wanafunzi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi vilivyopo Kurasini katika Manispaa ya Temeke Mkoani Dar es Salaam.

Kiwanda cha ushonaji ambacho kitawekwa vyerahani 200 kitakuwa na uwezo wa kuzalisha sare za Askari Polisi 800 kwa siku na kinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi, 2021 kwa gharama ya shilingi Milioni 666.4.

Ad

Jengo la ofisi na madarasa na jengo la bweni lenye ghorofa 5 yamejengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 799.6 ambapo kati ya fedha hizo shilingi Milioni 700 zilitolewa na Mhe. Rais Magufuli alipotembelea chuo hicho mwaka 2018.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IJP- Simon Sirro amesema katika awamu ya pili wanatarajia kujenga jengo la ofisi la ghorofa 5 kwa gharama ya shilingi Milioni 670 na bweni la ghorofa 6 kwa gharama ya shilingi Milioni 690 ili kukiboresha zaidi chuo hicho ambacho kilijengwa tangu mwaka 1958.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akitoka kukagua Majengo ya Madarasa ya Chuo cha Taaluma cha Polisi Kurasini mkoani Dar es Salaam mara baada ya kuyafungua leo tarehe 26 Februari 2021.

Amebainisha kuwa uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho uliofanywa kati ya mwaka 2015 na sasa umekiwezesha kuongeza uwezo wa kuchukua wanafunzi kutoka 440 hadi kufikia 625.

Akizungumza na Maafisa na Askari Polisi katika uwanja wa Polisi Kurasini, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kazi nzuri inayofanywa na Askari katika ulinzi wa raia na mali zao na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi yao pamoja na kuboresha mazingira yao ya kazi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene akizungumza mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuweka jiwe la msingi Ujenzi wa Kiwanda cha ushonaji Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi na kufungua Ofisi, Madarasa na Mabweni ya Chuo cha Taaluma cha Polisi Kurasini mkoani Dar es Salaam leo tarehe 26 Februari 2021.

Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na ujenzi wa kiwanda cha ushonaji ambacho kitasaidia kutatua tatizo la uhaba wa sare za askari na amepongeza kukamilishwa kwa majengo ya ofisi, maradasa na mabweni ambayo ameagiza yaanze kutumika mara moja.

Kutokana na kufurahishwa na jinsi Jeshi la Polisi lilivyofanikiwa kutumia shilingi Milioni 799 tu ikilinganishwa na shilingi Bilioni 1.4 ambazo zingetumika kama majengo hayo yangejengwa na wakandarasi, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa jeshi hilo ili zitumike kujenga majengo mengine ya kukiboresha zaidi chuo hicho, kikiwemo kituo cha afya ambacho IJP Sirro alieleza kuwepo mpango wa kukijenga ndani ya chuo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro akizungumza kwenye mkutano mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuweka jiwe la msingi Ujenzi wa Kiwanda cha ushonaji Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi na kufungua Ofisi, Madarasa na Mabweni ya Chuo cha Taaluma cha Polisi Kurasini mkoani Dar es Salaam leo tarehe 26 Februari 2021.

Rais Magufuli ameeleza dhamira yake ya kujenga vituo vya afya ama hospitali katika taasisi za majeshi hapa nchini akianzia na Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini ili kuondoa utaratibu wa Askari kwenda kutibiwa katika vituo vya afya ama hospitali za kiraia ambako hukutana na baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Kuhusu madai ya maafisa wastaafu wa polisi ambao hawajalipwa mafao yao, Mhe. Rais Magufuli ameeleza kushangazwa kwake na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutoshughulikia ipasavyo malipo hayo na ametoa wiki 1 kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene na IJP Sirro kuhakikisha wastaafu hao wanalipwa mafao yao.

Mabweni ya Chuo cha Taaluma cha Polisi Kurasini mkoani Dar es Salaam kama yanavyooekana mara baada ya kufunguliwa leo tarehe 26 Februari 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
Mabweni ya Chuo cha Taaluma cha Polisi Kurasini mkoani Dar es Salaam kama yanavyooekana mara baada ya kufunguliwa leo tarehe 26 Februari 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli

Kuhusu maombi ya Mbunge wa Temeke Mhe. Dorothy Kilave aliyeomba Manispaa ya Temeke isaidiwe kulipa deni la shilingi Bilioni 12.195 ambazo ni kati ya shilingi Bilioni 19 ilizokopa kutoka benki ya CRDB kwa ajili ya kulipa fidia ya maeneo ambayo manispaa hiyo iliyahitaji kwa ajili ya kujenga miradi, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haitalipa deni hilo na badala yake ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwenda kuchunguza sababu za kuomba mkopo huo na jinsi ulivyotumika kulipa fidia kwa kuwa zipo baadhi ya halmashauri ambazo hufanya hivyo kwa maslahi binafsi ya viongozi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *