HAKIKISHENI WATOTO WANAPATA TIBA SAHIHI PINDI WANAPOUGUA – MTAALAMU KUTOA PASS

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

Wazazi na walezi nchini wameshauriwa  kuwapeleka  watoto wao katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu stahiki pindi watakapoonesha viashiria  vyovyote vya ugonjwa.

Ad

Wito huo umetolewa leo na kiongozi wa kikundi cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha sekta ya kilimo Tanzania (Private Agricultural Sector Support-PASS) Elita Naimani walipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo kwa ajili ya kuchangia gharama za matibabu kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Kikundi cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS) wakimsikiliza mama ambaye mtoto wake amelazwa katika wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo walipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kulipia gharama za upasuaji kwa watoto wawili, kuwakatia kadi za bima watoto kumi pamoja na kutoa mahitaji madogo madogo kwa watoto waliolazwa katika wodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

Elita Naimani ambaye pia ni Meneja Rasilimali watu na Utawala wa PASS alisema katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani wameona ni vyema watembelee watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo ili wawajulie hali pamoja na kuwatia moyo mama zao wanaowauguza.

Alisema baada ya kuwatembelea watoto hao wameelezwa na wataalamu kuna baadhi yao wanasumbuliwa na maradhi ya moyo yanayotokana na bakteria wanaoshambulia  valvu za moyo (Rheumatic Heart Diseases).

“Tumeambiwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kuwa maradhi haya yanatokana na mtoto kuumwa homa ya mafindofindo (tonsillitis) kama mtoto hatapata matibabu sahihi au hatamaliza dozi bakteria hao watashambulia valvu za moyo na hivyo mtoto kuumwa maradhi hayo”,.

Meneja Rasilimali watu na Utawala kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania Elita Naimani akimkabidhi Mkuu wa Idara ya Watoto wenye magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Sulende Kubhoja kiasi cha Tsh. 4,540,000 kwa ajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wawili, kuwakatia kadi za bima watoto kumi katika wodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

“Hiki kitu kimenishtua sana kwani ni mara nyingi mtoto akiumwa unampa dawa ya maumivu pasipo kumpeleka hospitali. Ninawaomba wazazi wenzangu tuache tabia hii ukiona mwanao hayuko sawa Kiafya mpeleke hospitali kwa ajili ya matibabu na akipewa dawa hakikisha anakunywa kwa wakati na kumaliza dozi yote”, alisisitiza Elita.

Aidha katika kuchangia kwao gharama za matibabu ya watoto hao alisema waliona waiunge mkono kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake Duniani inayosema wanawake katika uongozi , chachu kufikia Dunia yenye usawa  kwa kutimiza ndoto za watoto kwa kuwachangia gharama za upasuaji, kuwakatia bima za afya pamoja na kuwapatia  mahitaji yao ya kila siku wawapo wodini.

Elita alisema, “Watoto hawa pamoja na kuwa wanapitia katika changamoto za ugonjwa wana ndoto zao kama ilivyo kwa watoto wengine hivyo basi tumekuja kuwasaidia kutimiza ndoto hizo  kwa kuwachangia gharama za matibabu ili wakipona waendelee na  maisha yao ikiwemo kusoma  kama ilivyo kwa watoto wengine”,.

Kikundi cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya Kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS) wakikabidhi zawadi za Huggies diapers, sabuni za unga za kufulia, dawa za meno, miswaki  na mafuta ya kupaka mwilini  kwa ajili ya matumizi ya  watoto waliolazwa  katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kiwete (JKCI) ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani.
Picha na: JKCI

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alikishukuru kikundi hicho cha wanawake kwa moyo wao wa upendo waliouonesha kwa watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo kiuchumi  kwa kuwachangia gharama za matibabu.

Prof. Janabi alisema matatizo makubwa ya moyo kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo ni matundu, mishipa ya damu ya moyo kutokukaa vizuri (Congenital Heart Diseases) pamoja na  maradhi ya moyo yanayotokana na bakteria wanaoshambulia valvu za moyo (Rheumatic Heart Diseases).

“Asilimia kubwa ya wagonjwa wetu wanatoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi na hivyo kushindwa kulipia gharama za matibabu. Tunawashukuru kwa mchango wenu ambao utaokoa maisha ya watoto hawa  na kuwarudishia  tabasamu kama ilivyo kwa watoto wengine”, alisema Prof. Janabi.

Akizungumza kwa niaba ya kinamama ambao watoto wao wamelazwa katika wodi hiyo Anganile Mwaisaka aliwashukuru wanawake hao kutoka PASS kwa kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto, kuwalipia bima za afya  pamoja na kuwapatia zawadi mbalimbali.

Kikundi hicho kimetoa shilingi milioni nne kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto wawili, Tshs. 540,000/= kwa ajili ya kulipia kadi kumi za bima ya afya kwa ajili ya watoto na kutoa zawadi za Huggies diapers, sabuni za unga za kufulia, dawa za meno, miswaki , mafuta ya kupaka mwilini  kwajili ya matumizi ya  watoto waliolazwa katika wodi hiyo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *