Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo alipokuwa akikabidhi hundi ya kiasi cha tsh takribani Bilioni 1.3, kwa ajili ya mikopo ya wanawake, walemavu na vijana robo ya nne, fedha zilizotengwa kwa bajeti ya mwaka 2021.
Amesema Kinondoni inaonesha dhamira ya dhati katika kuhakikisha inamkwamua mwanamke, kijana na mlemavu kiuchumi kwa kuwatengea fedha hizo za mikopo kwa wakati, kwa mujibu wa Sheria na kuwawezesha walengwa .
“Bilioni 3.4 kwa ajili ya mikopo kwa mwaka ni fedha nyingi zilizotengwa kwa bajeti ya 2021, hivyo kinamama, vijana na watu wenye ulemavu nafasi hii ni yenu, mnapopata fedha hizo mkazitumie kwa makusudi husika na si vinginevyo.” Amesema Daniel Chongolo.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bi Sipora Liana amesema kinamama ni jeshi kubwa katika kukuza uchumi wa familia hasa kunapokuwa na fursa za mikopo na kuwahakikishia haki na usawa katika suala hilo kwani ndiyo njia pekee ya kuwawezesha mikopo yenye tija, na kufanya miradi ya maendeleo na kuwataka kurejesha fedha hizo kwa wakati ili ziweze kusaidia na wengine.
Awali akitoa taarifa za mikopo na vikundi, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi.Halima Kahema amesema hadi sasa Kinondoni imeshakopesha fedha kwa vikundi 202, vinavyohusisha wanawake , vijana na watu wenye ulemavu.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Daniel Chongolo amaewataka wanawake,vijana na walavu kuhakikisha wanarejesha fedha hizo za mikopo kwa wakati ili ziweze kusaidia na wengine, na kuwasisitiza kutumia fedha hizo kwa makusudi kamili ili waweze kufikia tija inayokusudiwa.