SERIKALI YAANZISHA MADAWATI YA ULINZI KWA WATOTO MASHULENI


Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kuratibu uanzishwaji wa madawati ya Ulinzi wa Watoto katika shule za msingi na sekondari nchini.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii)  kwa kipindi Cha Julai,2020 hadi Februari, 2021.
Dkt. Gwajima amesema hadi kufikia Februari,2021 jumla ya madawati 182 yameanzishwa  na jumla ya wasimamizi wa madawati shuleni wapatao 360 walipatiwa mafunzo ya namna ya kusimamia madawati hayo ili kupunguza ukatili wa Watoto shuleni.
“Katika kutokomeza mila na desturi zenye madhara zinazosababisha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya Watoto nchini, Wizara tumetoa elimu kuhusu athari za Mila  hizo kwa Watoto, wananchi, walimu pamoja na viongozi wa kisiasa, dini na wale wa kimila katika Mikoa ya Mara,Geita,Tanga,Rukwa,Mbeya na Kigoma”. alisema Dkt. Gwajima
Kwa upande wa kutokomeza mimba za utotoni Dkt. Gwajima alisema wameweza kuwafikia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kuwapatia uelewa kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni kiafya, kielimu na kiuchumi pamoja na kuzuia ukatili mtandaoni.
Katika hatua nyingine ya taarifa ya utekelezaji ya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii hususan katika kuwawezesha Wanawake kiuchumi Dkt.Gwajima alisema  kupitia Sera ya Maendeleo ya Wanawake  na Jinsia ya mwaka 2000 pamoja na mkakati wake  wa utekelezaji  wa mwaka 2005, katika kipindi Cha  mwaka 2015  hadi 2020 kiasi cha shilingi Trioni 2.22 zimetolewa Kama mikopo na kunufaisha vikundi vya wanawake wajasiriamali takribani 490,000 vyenye wanawake zaidi ya milioni 4.9.
Alisema mikopo hiyo imetolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) kwa fedha zilizotengwa kupitia vyanzo vya ndani vya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo  kwa makundi ya wanawake(4%), vijana (4%) na watu wenye ulemavu (2%).

Ad

Unaweza kuangalia pia

Mitazamo ya Uongozi ya Mhe. Ummy Ally Mwalimu katika Sekta za Afya, Maendeleo ya Jamii, na Haki za Watoto

Ummy Ally Mwalimu ameonyesha mitazamo ya uongozi yenye mwelekeo wa kujali maendeleo na ustawi katika …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *