RAIS SAMIA AMEWATAKA VIONGOZI KUHAKIKISHA WANASIMAMIA MAJUKUMU NA WAJIBU WA WIZARA NA TAASISI ZAO IPASAVYO IKIWEMO UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KIMKAKATI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia mara baada ya kuwaapisha MAkatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumanne April 6, 2021
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, akizungumza na Viongozi na Watendaji mbalimbali kwenye Hafla ya kuapishwa kwa Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu na Makamishna wa Taasisi mbalimbali Ikulu Jijini Dar es salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan tarehe 06 Aprili, 2021 amewaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na wakuu wa taasisi aliowateua tarehe 04 Aprili, 2021.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Athman Kattanga, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Bw. Aboubakar Kunenge.

Ad

Akizungumza baada ya kuwaapisha, Rais Samia amewapongeza viongozi hao kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo na amewataka kwenda kuwatumikia Watanzania bila ubaguzi, kuzingatia haki na kujiepusha na dhuluma.

Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbalimbali wakila kiapo cha Maadili ya Utumishi wa Umma baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu April 6, 2021

Rais Samia amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia majukumu na wajibu wa wizara na taasisi zao ipasavyo ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati na miradi mingine kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/25.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimuapisha Bi. Grace Maghembe (Afya) kuwa Naibu Katibu Mkuu

Baadhi ya maelekezo aliyoyatoa ni kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya ikiwemo shule 26 za sekondari za wasichana, ujenzi na ukamilishaji wa hospitali, vituo vya afya na zahanati, kujaza nafasi 6,000 za walimu ambazo zipo wazi kutokana na walimu kustaafu, kuajiri watumishi wa afya na kununua vitendea kazi, kutumia mapato ya halmashauri kuboresha miundombinu ya barabara na amewataka viongozi wa Wilaya kutatua kero za wananchi vinginevyo kero hizo zikiibuka wakati wa ziara za viongozi wa Kitaifa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri wataondolewa katika nyadhifa zao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Bw. Gerald Musabila Kusaya kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu April 6, 2021

Rais Samia amewataka viongozi wa wizara na taasisi za Serikali kuondoa vikwazo na kero dhidi ya wawekezaji ikiwemo kuwanyima vibali vya watumishi wanaoruhusiwa kisheria kuwaajiri kutoka nje ya nchi, kuwawekea urasimu mkubwa wanapotaka kuwekeza ama kuendesha shughuli zao, kutokuwa na utozaji kodi unaotabirika na kutorudisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa wanaostahili kwani kufanya hivyo kumesababisha wawekezaji wengi kuondoka na wengine kutokuja kuwekeza hapa nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu April 6, 2021

Ameagiza miradi ya kimkakati isimamiwe vizuri, ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi unaosababisha tozo la riba na ongezeko la gharama za mradi ukomeshwe, kukuza uhusiano na Mataifa ya nje, kuratibu na kusimamia vizuri viwanda vinavyoanzishwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha kanda maalum za uwekezaji (EPZ) na kusimamia upatikanaji wa masoko ya mazao ya wakulima.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Bw. Allan Albert Kijazi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu April 6, 2021

Aidha, Rais Samia ametaka Wizara ya Madini iache kutumia nguvu katika uhusiano wa kiubia kati yake na kampuni za uchimbaji madini, iimarishe ulinzi wa madini ya Tanzanite ambayo yanaendelea kuibiwa licha ya kujengwa ukuta kuzunguka mgodi huo, kuhakikisha kitalu C cha ndani ya mgodi wa Mirerani hakiguswi na Wizara ya Maliasili na Utalii iache kuwazuia wachimbaji madini katika maeneo ya hifadhi ambayo yameonekana kuwa na madini hayo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Godius Walter Kahyarara kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu April 6, 2021

Ametaka maelekezo ya Ilani ya kufikisha maji vijijini kwa asilimia 85 na mijini kwa asilimia 95 ifikapo 2025 yatekelezwe, vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe na kutakiwa kuzingatia sheria, mfumo wa elimu uangaliwe ili uwaandae vijana wanaoweza kujiajiri, masomo ya historia na Kiswahili yatiliwe mkazo, Madaktari wapate motisha, bima ya afya kwa wote itekelezwe na dawa zipatikane vituoni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Bw. Gabriel Joseph Migire kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (anayeshughulikia uchukuzi) katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu April 6, 2021

Kuhusu ugonjwa wa Korona (Covid-19), Mhe. Rais Samia amesema ataunda timu ya wataalamu itakayoangalia na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya nini kinapaswa kufanyika ili Tanzania isiwe pekee yake katika juhudi za kukabiliana na janga hilo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Kheri Abdul Mahimbali kuwa Naibu Katib u Mkuu Wizara ya Nishati katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu April 6, 2021

Maeneo mengine aliyoyatolea maelekezo ni kuimarisha uvuvi na mifugo, kufuatilia utekelezaji wa miradi mikubwa kama vile mradi wa usindikaji gesi asilia (LNG), ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa Msalato Dodoma, ujenzi wa barabara za mzunguko za Dodoma, ujenzi wa Bwawa la Nyerere, kunusuru Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na amesema atazifuatilia kwa ukaribu taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo (TCRA, NSSF, PSSSF, TPA na TASAC).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Bw. Alphayo Japani Kidata kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu April 6, 2021
Ad

Unaweza kuangalia pia

Askofu Dkt Maasa OleGabriel RAIS SAMIA ANATEKELEZA MAAGIZO YA MUNGU YA KUITUNZA BUSTANI YA EDENI

Askofu Dkt. Maasa OleGabriel Katibu Mkuu Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania na Askofu wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *