Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imewahukumu kifungo cha miaka 30 gerezani washtakiwa Damian Jankowsky Krzysztof raia wa Poland na mke wake Eliwaza Raphael Pyuza Mtanzania kwa makosa ya kulima mimea 729 ya bangi na kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kiasi cha kilogramu 17.2 kinyume cha sheria.
Vilevile, Mahakama hiyo imewahukumu kifungo cha miaka mitatu gerezani au kulipa faini ya shilingi milioni nne kila mmoja washtakiwa Eliwaza Raphael Pyuza, Hanif Hassanali Kanani raia wa Tanzania mwenye asili ya kihindi na Boniface George Kessy Mtanzania, baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kutumia dawa za kulevya aina ya bangi.
Hukumu hiyo imetolewa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mhe. Bernazitha Maziku wa Mahakama hiyo baada ya ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo kuthibitisha kwamba, washtakiwa wanajihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Sambamba na hukumu hiyo, Mahakama imetoa amri ya kutaifishwa kwa shamba hekari moja na nusu lililopo eneo la Himo njia panda, pesa taslim shilingi 26,765,000/= alizokamatwa nazo Damian, Madiaba mawili yaliyokutwa na bangi, na pikipiki aina ya KTM Adventure yenye namba za usajili MC 972 AAD.
Pia Mahakama imeamuru kuteketezwa kwa simtank mbili za lita 2000 zilizokuwa zikitumika kumwagilia miche ya bangi kwenye shamba eneo la Himo na kiasi chote cha bangi kilichokamatwa.
Katika shauri hilo, upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Ignas Mwinuka, Verdiana Mlenzana na Lilian Kowero. Upande wa utetezi uliongozwa na wakili wa kujitegemea FaiyGrace Sadala ambae aliwatetea Damian, Eliwaza na Hanif huku mstakiwa wa nne Boniface Kessy akijitetea pekeyake.
Washtakiwa, walikamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) tarehe 08 mwezi Februari 2020 eneo la njia panda ya Himo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, na kufunguliwa kesi ya jinai namba 79 ya mwaka 2020.
Washtakiwa wametiwa hatiani na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya Mwaka 2015 kama ilivyorejewa Mwaka 2019