WAZIRI WA NISHATI APONGEZA WAFANYAKAZI KWA KUCHANGIA UCHUMI WA KATI

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amewapongeza wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kufanya kazi kwa ufanisi ambao umechagiza nchi kuingia katika uchumi wa kati kutokana na uwepo wa nishati inayotabirika.

Dkt.Kalemani ametoa pongezi hizo jijini Dodoma, tarehe 5 Mei, 2021 wakati akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati ambapo Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti, Kheri Mahimbali ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara, Mhandisi Leonard Masanja.

Ad

“Wizara ya Nishati ni injini katika uchumi wa Taifa letu, huwezi kuzungumzia maendeleo bila kugusa masuala ya nishati, na nishati si umeme tu, bali kuna gesi, mafuta na nyinginezo, ujenzi wa uchumi wa viwanda vikubwa  na vidogo unategemea nishati kama vile ya umeme ambayo inachochea kwa haraka katika kujenga viwanda ambavyo vinasisitizwa katika uchumi huu wa kati.” Amesema Dkt.Kalemani

Mwenyekiti wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Kheri Mahimbali akieleza umuhimu wa Kikao cha Baraza la Wafanayakazi wa Wizara hiyo kilichofanyika Mei 5, 2021 Jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa, utendaji mzuri wa wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake umepelekea wananchi wengi kutumia umeme ambapo kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati hiyo, na hii inatokana na juhudi zinazofanywa na wafanyakazi hao.

Mbali ya pongezi hizo, Waziri wa Nishati amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi wenye weledi ili kuendelea kupata mafanikio na kujenga uchumi imara.

Aidha, amewaasa kuendelea kudumisha ushirikino kati ya Mfanyakazi na Muajiri  na kufanya kazi kwa  kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ili kuongeza ufanisi.

Vilevile, amewasisitiza viongozi wa Wizara kuzingatia maslahi ya wafanyakazi ikiwemo kupandisha vyeo, madaraja na kulipa mafao ili kuwapa morali wafanyakazi ya kuchapa kazi zaidi.

Afisa Elimu Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Tulia Msemwa akiwasilisha mada wakati wa kikao cha Baraza la Wafanayakazi wa Wizara ya Nishati kilichofanyika Mei 5, 2021 Jijini Dodoma.

Kwa upande wa wafanyakazi, alitoa angalizo la kutokufanya kazi kwa mazoea na badala yake kila mfanyakazi anapaswa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, kujituma, kasi na kuzingatia viwango.

Kuhusu masuala ya kipaumbele ya kimkakati yaliyopangwa na Wizara, ikiwemo utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (MW 2115), ameagiza kuwa, yatekelezwe kwa wakati na Baraza la Wafanyakazi lihakikishe kuwa masuala hayo yanatekelezeka.

Aidha ameagiza kuwa, Baraza hilo lijadili na kutoa maoni kuhusu ufanikishaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya usambazaji umeme katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ya vijiji,  miradi ya gesi ukiwemo wa Kuchakata na Usindikaji Gesi asilia (LNG),  mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika Reli ya Kisasa (SGR).

Watumishi wa Wizara ya Nishati wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nishati wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanayakazi wa Wizara hiyo kilichofanyika Mei 5, 2021 Jijini Dodoma.

Teresia Mhagama, Dodoma

Dkt. Kalemani amesisitiza pia, kuhusu wananchi kupewa elimu ya matumizi ya umeme huku akitolea mfano kuwa kuna baadhi ya maeneo, Serikali inatumia fedha nyingi kupekeleka miradi ya umeme lakini wananchi wanaounga umeme si wengi kutokana na ukosefu wa uelewa wa matumizi ya nishati hiyo.

Awali, Mwenyekiti wa Mkutano huo, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, alisema kuwa Muundo wa Baraza hilo la Wafanyakazi lina wajumbe wapatao 50 wanaotoka makundi mbalimbali na kwamba  baadhi  ya kazi mahsusi za Baraza hilo ni kujadili na kupitisha mpango wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Alitaja baadhi ya kazi nyingine za Baraza hilo kuwa ni, kujadili taarifa ya utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi, miradi ya umeme na nishati mbadala inayoendelea pamoja na mipango ya maendeleo kwa mwaka 2021/2022.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE, Tawi la Wizara  ya Nishati, Zghambo Chinula, aliipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Nishati na pia, alitumia fursa hiyo kueleza masuala mbalimbali yanayohusu Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati ikiwemo ya upandishaji madaraja na stahili mbalimbali.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *