PROGRAMU TUMIZI YA SIMU ZA MKONONI (MOBILE APP) YA MFUMO WA ANWANI NA POSTIKODI YATAMBULISHWA KWA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI NA MAKATIBU TAWALA WA MIKOA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula na timu yake ya wataalamu wametoa wasilisho la programu tumizi ya simu za mkononi (Mobile App) ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi pamoja na hatua iliyofikiwa ya usimikaji wa Mfumo huo nchini kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Makatibu Tawala wa Mikoa katika Mkutano wa 11 wa Maboresho ya Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa (TOA).

Akizungumza katika mkutano huo jijini Dodoma, Dkt. Chaula amesema kuwa Wizara hiyo inatekeleza ujenzi na usimikaji wa Mfumo huo kupitia Halmashauri zote nchini ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/21 halmashauri 13 ziliingizwa kwenye mpango wa kusimikwa mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi.

Ad
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula akionesha Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi wakati Wizara hiyo ikitambulisha programu tumizi ya simu za mkononi (Mobile Application) ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa Wakurugenzi wa halmashauri na Makatibu Tawala wa mikoa katika Mkutano wa 11 wa TOA uliofanyika jijini, Dodoma

Ameongeza kuwa mpango wa Wizara hiyo ni nyumba zote nchini ziwe na Anwani za Makazi ifikapo June 2022 na kuzipongeza halmashauri za mji wa Bukoba na Jiji la Mwanza kwa kuwa vinara wa utekelezaji wa Mfumo huo

“Ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya Mfumo huu Wizara imetengeneza programu tumizi ya simu ya mkononi (mobile application) ambayo itawezesha kutambua na kuonesha nyumba ilipo au popote mwananchi anapotaka kwenda na pia utarahisisha shughuli za biashara”, alizungumza Dkt. Chaula

Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu akimkabidhi Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Tina Sekambo wakati Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikitambulisha programu tumizi ya simu za mkononi (Mobile Application) ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa Wakurugenzi wa halmashauri na Makatibu Tawala wa mikoa katika Mkutano wa 11 wa TOA uliofanyika jijini, Dodoma

Akizungumzia mwongozo wa utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi, Dkt. Chaula amesema kuwa mwongozo huo umefanyiwa maboresho na utagawanywa kwa wadau kwa sababu utekelezaji wake unahusisha Wizara zaidi ya moja ikiwemo TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu kama Serikali na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikiwa kama sekretarieti.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo ameizungumzia programu tumizi ya Mfumo huo kuwa na manufaa mengi kiuchumi na kijamii hasa katika dhana nzima ya uchumi wa kidijitali ambapo mfumo huo utarahisisha shughuli za kiuchumi kuweza kufanyika kidijitali.

Mkurugenzi Idara ya Mawasiliano wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza akiwasilisha utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi wakati Wizara hiyo ikitambulisha programu tumizi ya simu za mkononi (Mobile Application) ya Mfumo huo kwa Wakurugenzi wa halmashauri na Makatibu Tawala wa mikoa katika Mkutano wa 11 wa TOA uliofanyika jijini, Dodoma

Ameongeza kuwa chimbuko la mfumo huo ni Sera ya Taifa ya Posta inayoelekeza kuwa na Anwani ya Makazi ili kuweza kufikishiwa huduma mahali mwananchi alipo na kuongeza manufaa ya kijamii, kiuchumi na pia kimataifa ambapo nchi ya Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Posta Afrika.

Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Gerald Mweli akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi wakati Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikitambulisha programu tumizi ya simu za mkononi (Mobile Application) ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa Wakurugenzi wa halmashauri na Makatibu Tawala wa mikoa katika Mkutano wa 11 wa TOA uliofanyika jijini, Dodoma
Baadhi ya Wakurugenzi wa halmashauri na Makatibu Tawala wa mikoa wakifuatilia wasilisho la kuitambulisha programu tumizi ya simu za mkononi (Mobile Application) ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi lililofanywa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika Mkutano wa 11 wa TOA uliofanyika jijini, Dodoma

Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma

Naye Mhandisi Jampyon Mbugi wa Wizara hiyo amezungumza na wajumbe wa Mkutano huo na kuwaomba kila mmoja kutimiza wajibu wake na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kurahisisha zoezi zima la usimikaji wa majina ya barabara, mitaa na namba za nyumba pamoja na ukusanyaji wa taarifa za makazi.

Aidha, wataalamu wa programu tumizi ya mfumo huo waliitambulisha program hiyo kwa wajumbe wa kikao hicho na kuonesha namna ya kuingia katika program hiyo na jinsi ya kuitumia ambapo inaonesha njia na barabara ya kupita mpaka kufika mahali ambapo mtumiaji anataka kufika.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *