Na Mwandishi wetu, Dar
Shirikisho la Urusi limesema linaunga mkono jitihada zinazofanywa na Umoja wa Afrika katika kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo kwa kuwa matatizo ya Afrika yanahitaji kutatuliwa na Waafrika wenyewe bila kuingiliwa na Mataifa mengine.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe Maalum wa Rais wa Shirikisho Urusi kuhusu masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati Mhe. Mikhail Bogdanov ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) na kupongeza jitihada zinazofanywa na Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kutatua changamoto za kiusalama katika eneo la maziwa makuu.
“Tunaunga mkono jitihada zinazofanywa na Umoja wa Afrika katika kutatua changamoto zinazolikabili Afrika kwa kuwa matatizo ya Afrika yanahitaji kutatuliwa na Waafrika wenyewe,” amesema Bogdanov. Pia Naibu waziri huyo amepongeza jitihada zinazofanywa na Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kutatua changamoto za kiusalama katika eneo la maziwa makuu.
Aidha, Bogdanov ameongeza kuwa Urusi ni moja kati ya nchi zinazoamini kuwa Afrika inaweza kutatua matatizo yake bila ya kuingiliwa kutokana na mazingira yaliyopo na kwamba nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Afrika hususani Tanzania katika kuleta amani na usalama sambamba na kuchochea jitihada za maendeleo ikiwemo biashara na uwekezaji.
Kwa upande wake waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amemuomba Waziri huyo kuimarisha zaidi mahusiano ya diplomasia ya Uchumi hususani katika sekta ya biashara na uwekezaji kutokana na takwimu zilizopo kuonesha kiwango kidogo cha mahusiano ya kibiashara na uwekezaji.
“Tumejadili masuala la kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Urusi hasa katika sekta ya biashara na uwekezaji, ambapo Mhe. Bogdanov ameahidi kulifanyia kazi suala hilo na kuhakikisha kuwa tunakuza biashara na uwekezaji,” amesema Balozi Mulamula
Pia Balozi Mulamula amesema Tanzania iko tayari kuwa mwenyeji wa mkutano wa ushirikiano kati ya Urusi na Afrika ambao umepangwa kufanyika Afrika ambapo Umoja wa Afrika unajukumu la kupendekeza nchi moja ambayo itakuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Amemuomba pia Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi kuhamasisha watalii kutoka Urusi kuja kwa wingi hapa nchini na kwamba licha ya ugonjwa wa COVID 19 Tanzania imechukua tahadhari zote zinazosisitizwa na Shirika la Afya Duniani.