SERIKALI KUNUNUA TANI 90,000 ZA MAHINDI KWA WAKULIMA

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo tarehe 14 Septemba 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa kuhusu ununuzi wa mahindi Mwingine pichani ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA Ndg Milton Lupa (Kulia)

Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda amesema  kwa sasa mahindi yatanunuliwa tani 90,000 ambapo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) utaanza kununua kwenye mikoa saba kwa bei ya sh. 500 kwa Kilogramu huku Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) ikinunua mikoa sita kwa bei ya soko.

Alitaja mikoa saba ambayo NFRA itaanza kununua mahindi hayo kuwa ni pamoja na Ruvuma, Rukwa, Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Iringa huku CPB ikinunua mikoa sita ambayo ni Rukwa, Katavi, Njombe, Songwe, Dodoma na Manyara.

Ad

Hayo ameyasema jijini Dodoma leo tarehe 14 Septemba 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa Tsh Bilioni 50 kwa ajili ya kuiwezesha NFRA kununua mahindi kwa wakulima hasa wadogo.

Amesema zoezi la kununua mahindi tayari lilitangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya Rais Samia kuidhinisha sh. Bilioni 50 kwa kazi hiyo.

Amebainisha kuwa mwaka huu zimezalishwa tani milioni sita za mahindi huku ziada ikiwa mara mbili ya uzalishaji uliofanyika kwa mwama uliopita huku nchi za Zimbabwe, Zambia zikitajwa kuzalisha kwa wingi nafaka hiyo.

“Lazima tutoe tahadhari kwa maana mwakani bei inaweza kupanda lakini kwakuwa kuna mikoa inaongoza kwa uzalishaji hapa nchini kama Ruvuma ikifuatiwa na Rukwa bei ni ndogo sana wakati mkoa wa Katavi, Songwe zikiwa chini zaidi hali inayompeleka mkulima kushindwa kupata fedha za kujikimu na kujiandaa kwa msimu ujao”

“Tayari NFRA wamepewa fedha za kununua na tayari zimeanza kuingia hizi ni fedha za serikali zilitolewa kwa kazi hiyo hivyo NFRA wataanza kununua mahindi katika mikoa saba huku CPB ikinunua mikoa sita,” Amekaririwa Waziri Mkenda

Amesema mahindi hayo yatanunuliwa kupitia Vyama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) au vikundi vya wakulima vilivyosajiliwa na kwa wakulima wadogo kwa magunia yasiyozidi 300 au tani 30 kwakuwa wanataka rekodi ya kila mkulima aliyelima mahindi yanunuliwe na fedha zilizotolewa na Serikali zitumike kama ilivyokusudiwa.

Amesema baada ya zoezi hilo kufanyika wizara itafanya ufuatiliaji kwa viongozi wa mikoa ili kupata taarifa na namna mgawanyo wa ununuzi ulivyofanyika kwenye mikoa tajwa.

“Tutakagua hivyo wananchi au wakulima  mkiona dalili za ukiukwaji wa ununuzi wa mahindi toeni taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo kwenye maeneo yenu,” amebainisha.

Afisa Mtendaji Mkuu NFRA, Milton Lupa amesema wanaenda kununua nafaka hiyo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwenye mikoa ya Songea, Ruvuma, Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa kupitia AMCOS na wakulima waliosajiliwa.

“Wananchi watulie tutanunua mahindi, wapunguze vurugu kwakuwa tutafuata utaratibu uliowekwa tunawahakikishia tutawafikia wakulima wenye kipato cha chini wenye mahindi yanayokidhi vigezo,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu CPB, Dkt Anselim Moshi amesema watanunua mahindi hayo kama walivyoelekezwa na wizara na kwamba wameshaanza kutafuta masoko nje ya nchi  mbalimbali zikiwemo  Kenya, Sudani Kusini, Comoro, Burundi na Rwanda.“Tumetafuta fedha kwa kukopa kwenye benki tutanunua nafaka hiyo kwa wingi na kusafirisha nje ya nchi ambapo ndio tumetafuta masoko kwa ajili ya kuuza, ”amesema.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Makamu wa Rais Dkt. Mpango Awakaribisha Wawekezaji Katika Nishati ya Jotoardhi Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *