Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, tarehe 23 Septemba, 2021 amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa katika uongozi wake, Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na mataifa na wadau wengine duniani kutatua changamoto zinazoukabili ulimwengu hivi sasa.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia ameeleza kuwa ugonjwa wa Virusi vya Korona, (UVIKO 19) bado unaendelea kupunguza kasi ya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika muda uliopangwa na kwamba kwenye baadhi ya nyanja, taarifa zinaonesha kuwa kumekuwa na athari zilizorudisha nyuma mafanikio yaliyokwishapatikana.
Rais Samia ametolea mfano kuwa takriban watu milioni 71 duniani wanatarajiwa kurejea katika umasikini licha ya kwamba walikwishaondokana na hali hiyo na kusisitiza kuwa iko haja ya kuunganisha juhudi za kubadili hali hiyo hasa kwa kuwa changamoto za janga hilo hazijali hali ya nchi ilivyo.
Aidha, Rais Samia amezishukuru Taasisi za Kimataifa ikiwemo Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa jitihada zao za kusaidia nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zisiathirike zaidi kiuchumi.
Vilevile, ameeleza kuwa tangu kuanza kwa UVIKO 19, Tanzania imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali kukabiliana nao ambapo mwezi Julai, 2021 alizindua rasmi programu ya chanjo nchi nzima na kutoa wito kuwa ili watu wengi katika nchi zinazoendelea waweze kupata chanjo, ni vyema hakimiliki ya kuzalisha chanjo hizo itolewa ili uzalishaji ufanyike kwenye nchi nyingi.
Rais Samia ametumia hotuba hiyo pia kueleza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi licha ya changamoto za ugonjwa huo na kwamba baada ya kushuka kwa ukuaji uchumi kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 5.4 hivi sasa Tanzania inafanya jitihada za kuziinua sekta zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo, hususan utalii, na pia kuimarisha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji nchini pamoja na kuimarisha misingi ya utawala bora.
Halikadhalika, Rais Samia ameeleza jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika nyanja za uchumi ikiwa ni pamoja na kuweka sera madhubuti na maboresho ya mfumo wa bajeti ili kupunguza idadi ya wanawake na wasichana wanaoishi katika umasikini.
Rais Samia amezungumzia pia athari za mabadiliko ya Tabia Nchi na umuhimu wa kuchukua hatua za kukabiliana na janga hilo na kuyasisitiza mataifa yaliyoendelea kutimiza ahadi zao za kutoa Dola za Kimarekani bilioni 100 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025 kama ilivyokubaliwa katika Azimio la Paris.
Wakati huo huo, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya Grumeti Mikael Andrea anayemuwakilisha mmiliki wa Makapuni hayo Bw. Paul Tudor Jones II ambapo amempongeza Mhe. Rais kwa kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania.
Bw. Mikael Andrea amesema kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania, makampuni yao yataendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania kwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii.
Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amewashukuru Wawekezaji hao kwa uamuzi wao wa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya utalii nchini Tanzania.
Aidha. Rais Samia pia amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Antonio Guterres na kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo ulinzi na usalama barani Afrika, athari za UVIKO 19 kiuchumi na kijamii pamoja na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Rais Samia amempongeza Mhe. Guterres kwa kuchaguliwa kwa mara ya pili kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kumteua tena Bi. Amina J. Mohamed kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo.