WAZIRI NDAKI ATEKELEZA AGIZO LA RAIS, AGAWA ENEO KWA WAFUGAJI

Na. Edward Kondela

Serikali imekabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza eneo lenye ukubwa wa Hekta 6,000 lililotolewa kwa wananchi wa vijiji vya Mpeta na Chakuru ili ligawiwe kwa wananchi hao kwa ajili ya shughuli za ufugaji baada ya mgogoro wa muda mrefu wa wananchi hao kuvamia Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya Malai iliyopo Mkoani Kigoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amekabidhi eneo hilo (23.09.2021), akitekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameamua eneo hilo kumegwa kutoka Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya Malai baada ya kusikia kilio cha wafugaji hao kutoka mikoa ya kanda ya ziwa kutokuwa na maeneo kwa ajili ya mifugo yao.

Waziri Ndaki amebainisha kuwa hatua hiyo inakuja kukiwa na mgogoro mkubwa baina ya wananchi hao ambao ni wafugaji, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambapo wananchi zaidi ya 5,900 wamevamia eneo la ranchi hiyo kitongoji cha Mwanduhu Bantu kijiji cha Mpeta na eneo la Kazaroho Wilaya ya Uvinza na kuendesha shughuli za ufugaji na kilimo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama kushoto) akitoa maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe kuhusu ugawaji wa eneo la Hekta 6,000 lililomegwa kutoka kwenye Ranchi ya Taifa ya Malai katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma na kugawiwa kwa wafugaji waliovamia eneo hilo. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Kabla ya hatua ya kukabidhi eneo hilo serikali kupitia Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi, watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Uvinza na Kasulu kutoka Idara za Ardhi, Kilimo na Mifugo ambao walifanya sensa ya kujua idadi ya wavamizi hao kupima eneo ambalo litaweza kutumika kwa wananchi, kuchora ramani upya na kugawa eneo kuondoa mgogoro huo mchakato uliochukua miezi miwili kukamilika.

Waziri Ndaki amesema awali Rais Samia alishauriwa kutoa Hekta 4,000 lakini baada ya kufanywa kwa sensa ya watu na mifugo aliamua kutoa Hekta 6,000 ili ziweze kutumiwa na wananchi hao.

“Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa eneo hili naomba kutangaza kuwa serikali haitaongeza eneo lingine na mgawanyo utafanywa kwa watu zaidi ya 5,900 waliokuwa wakihusika na mgogoro na kwamba watakaovamia eneo la ranchi ambalo siyo eneo lililomegwa na kugawiwa sheria itachukua mkondo wake.” Amesema Waziri Ndaki

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe (aliyesimama kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza Bw. Masumbuko Kechegwa (aliyesimama kushoto) wakikabidhiana nyaraka ambapo NARCO imekabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Hekta 6,000 zilizomegwa kutoka kwenye Ranchi ya Malai kwa ajili ya wananchi ambao ni wafugaji waliovamia ranchi hiyo. Agizo la kumegwa eneo hilo limetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Akitoa taarifa kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe amesema mchakato umefanyika kwa kuwa na vikao zaidi ya vitano na viongozi na wananchi waliovamia eneo hilo ambapo changamoto mbalimbali zilijitokeza.

Prof. Msoffe amesema licha ya mapendekezo na ushauri uliokuwa ukitolewa na wataalam wananchi hao pia walikuwa na mapendekezo, ushauri na maamuzi ambayo wakati mwingine yaliegemea kwenye baadhi ya makundi kuona yananufaika zaidi hivyo maamuzi mengi kuwa na changamoto ya kufikia mwisho kwa faida ya wote.

“Kwa sasa kumekuwa na idadi kubwa sana ya watu na mifugo na hiyo inatokana na ongezeko kubwa la wavamizi hao ambapo baada ya kusikia kumeanza mchakato wa sensa na upimaji baadhi ya watu waliongezeka ambao hapo awali hawakuwepo kwenye eneo hilo na wengine wameingia kwenye eneo ambalo hapo awali halikuwa kwenye mgogoro na kuanza kudai waongezewe eneo.” Alisema Mkurugenzi huyo wa NARCO.

Ameongeza kuwa eneo hilo la Hekta 6,000 limegawanywa kwa Hekta 2,500 kutoa kitongoji cha Kazaroho kijiji cha Mpeta na Hekta 3500 kitongoji cha Mwanduhu Bantu kijiji cha Mpeta wilaya ya Uvinza.

Naye Mkuu wa Wilaya Uvinza, Anafi Msabaha akizungumza katika mkutano huo amesema mgogoro huo umefikia mwisho kwa maamuzi ya Rais kutoa eneo ambalo litatumiwa na wananchi waliokuwa kwenye mgororo na kwamba wilaya itasimamia kuona taratibu za ugawaji zinafanyika kwa uwazi na wananchi ambao ni wafugaji waliohusika wanapatiwa maeneo kulingana na mgawanyo utakaofanyika.

Baadhi ya wananchi walioongea baada ya taarifa ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki kuhusu kutolewa kwa eneo hilo wameishukuru serikali kwa kukubali kuwamegea eneo hilo, huku wakidai bado eneo walilopewa haliwezi kutosheleza mahitaji na kuomba waongezewe maeneo zaidi.

Mmoja wa wananchi hao Bw. Masele Mayenga amesema eneo lililotolewa linaweza kutumika kupatia ufumbuzi wa mgogoro uliokuwepo ambapo wafugaji walikuwa wakisumbuliwa na kuondolewa eneo la Ranchi kwa kuvamia eneo hilo ambapo amesema kuwa bado eneo walilopewa haitoshelezi mahitaji yao.

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMSHUSHA MAMA NDOO KICHWANI – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilwa, kufanya utafiti wa kina …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.