BENKI YA DUNIA YAJA NA NEEMA KWA TANZANIA

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akieleza kuhusu suala la ajira kwa vijana wakati wa mkutano na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem (hayupo pichani), jijini Dodoma.

Benki ya Dunia imeahidi kuisaidia Tanzania kukabiliana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO – 19 pamoja na kusaidia kutekeleza miradi itakayosaidia kukuza ajira kwa vijana, kuboresha miundombinu ya afya na elimu pamoja na kuendeleza rasilimali watu.

Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Makamu wa Rais wa Benki hiyo, Dkt. Hafez Ghanem alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

Ad

Aliyataja maeneo muhimu yatakayosaidia kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira hususan kwa vijana kuwa ni pamoja na kuwekeza katika mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), kuimarisha sekta ya nishati ya umeme, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuimarisha sekta binafsi ili iweze kuchangia katika kutoa ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB) Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, akieleza nia ya WB kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kupambana na umasikini wakati wa mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), jijini Dodoma.

“Tumejadiliana mambo mengi lakini suala la muhimu ni kuhakikisha sekta binafsi inawekewa mazingira mazuri ya kuwekeza katika miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi ikiwemo nishati, kukuza ajira, pamoja na kuwekeza kwenye maeneo yatakayosaidia kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na suala zima la elimu” alisema Dkt. Ghanem.

Ili kutimiza azma hiyo, Dkt. Ghanem aliishauri Serikali kuangalia namna ya kuboresha sera na sheria zitakazochochea wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza mitaji na technolojia vitakavyochochea mapinduzi ya viwanda kupitia mfumo wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusimamia vizuri masuala ya uchumi licha ya kuwepo kwa changamoto ya ugonjwa wa UVIKO -19 ikilinganishwa na nchi nyingine ambapo kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kimefikia wastani wa asilimia 4.6.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem (katikati) na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Mhe. Mara Warwick, wakiteta jambo baada ya mkutano wao uliofanyika jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru benki hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi mitano iliyosainiwa hivi karibuni inayogharimu zaidi ya shilingi trilioni 1.3.

Dkt. Nchemba alisema hadi sasa benki hiyo imewekeza zaidi ya dola bilioni 5.5 kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo na kuishuru benki hiyo kwa ahadi ya kuendeleza ushirikiano katika kuendeleza miradi mingine mipya ya kimkakati ikiwemo kuboresha Jiji la Dar es Salaam pamoja na Miji mingine 45 nchini.

“Leo tumeongelea maeneo mengine mawili ya Mkakati wa Maendeleo ambapo tumekubaliana kuweka nguvu kubwa katika kukuza Sekta Binafsi inayolenga kutengeneza ajira nyingi kwa vijana na mpango wa kuwawezesha wanafunzi wengi kupata elimu bila kuacha masomo” alisema Dkt. Nchemba.

Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Mara Warwick, akifafanua jambo wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem (kushoto), jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem (katikati) na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Mara Warwick, wakiteta jambo baada ya kumalizika kwa mkutano wao uliofanyika jijini Dodoma.

Na. Farida Ramadhan na Josephine Majura WFM- DODOMA

Aliihakikisha Benki ya Dunia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika masuala mbalimbali ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika nchi kwa haraka zaidi.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB), Dkt. Hafez Ghanem, yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku 4 ambapo anatarajia kukutana na viongozi mbalimbali wa nchi ili kujadiliana kuhusu masuala ya ushirikiano kati ya Benki hiyo na Tanzania, changamoto zinazoikabili Tanzania na fursa zilizopo ndani ya Benki hiyo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *