Rais Samia Suluhu Hassan, ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuongeza uwazi na uwajibikaji katika kazi zao pamoja na kwenda sambamba na vipaumbele na mipango ya Serikali ili ziweze kuleta tija katika jamii.
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 30 Septemba, 2021 wakati akihutubia katika Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Mhe. Rais Samia amesema kwa sasa Serikali inatekeleza Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2026) hivyo ni vyema Mashirika hayo kuandaa mipango yake kwa kuoanisha na mpango huo wa Serikali.
Aidha, Rais Samia ameyataka Mashirika hayo Yasiyo ya Kiserikali hususan ya ndani pamoja na Wizara husika kuandaa mpango mkakati utakaosaidia Mashirika hayo kuondokana na utegemezi katika utendaji wa kazi zao.
Mhe. Rais Samia ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufanya kazi zinazoendana na mila, utamaduni, desturi na maadili ya kitanzania pamoja na kusimamia sheria zinazoongoza Mashirika hayo.
Vilevile, Mhe. Rais Samia ameyaomba Mashirika hayo kufanya kazi pamoja na Serikali katika kuwaelimisha wananchi kuhusu kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 2022, na kuwapa wananchi elimu ya tahadhari za kujikinga na UVIKO 19.
Katika mkutano huo, Mhe. Rais Samia amezindua Taarifa ya mchango wa Mashirika hayo Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo ya Taifa.
Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia, ameongoza waombolezaji kuuaga mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Marehemu William Tate Ole Nasha.
Shughuli za kuaga mwili wa Marehemu Ole Nasha zimefanyika katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, Katibu Mkuu wa CCM, Ndg. Daniel Chongolo, Mawaziri na Manaibu Mawaziri, Wabunge pamoja na viongozi wengine wa vyama vya Siasa na Serikali.