WAZIRI NDAKI ABAINISHA UFUGAJI WA SAMAKI KUONGEZA MALIGHAFI VIWANDANI

Na. Edward Kondela

Serikali imesema uwekezaji wa ufugaji wa samaki utasaidia kuongeza malighafi kwenye viwanda vya uchakataji wa samaki pamoja na kuanzisha viwanda vipya hususan katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Ad

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema hayo (02.10.2021) wakati alipotembelea shamba la ufugaji samaki linalomilikiwa na Kampuni ya Tanlapia lililopo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya kuona shughuli zao za ufugaji wa samaki na namna wadau ambao serikali inataka wafanikiwe katika ufugaji wa samaki ili kufikia lengo la kuzalisha samaki kwa wingi ifikapo mwaka 2025 na kufikia kiwango sawa cha samaki wanaovunwa kupitia maji ya asili.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanlapia inayomiliki shamba la kufuga samaki aina ya sato katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani, Bw. Baraka Karangahe (Kushoto) akimuelezea Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka wizarani Dkt. Nazael Madala kuwa lengo la mradi ni soko la hapa nchini ili kila mwananchi aweze kupata samaki kwa bei nafuu na kuishukuru serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano kwa wawekezaji hapa nchini. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

“Kwa sasa tuna viwanda vingi kidogo na vingine vinazalisha chini ya viwango kutokana na kukosa malighafi, sasa uzalishaji kama huu utasaidia viwanda kuwa na malighafi hususan katika ukanda wa bahari ambao una viwanda vichache vya kuchakata mazao ya samaki na bado tunataka uzalishaji huu uendelee ili kuzalisha viwanda ambavyo tayari vimesimikwa katika ukanda wa bahari na kusafirisha bidhaa za samaki nje ya nchi.” Amesema Mhe. Ndaki

Waziri Ndaki ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuhakikisha inaendeleza wawekezaji hapa nchini ili kufikia malengo ya uzalishaji mkubwa wa samaki kupitia ufugaji wa samaki.

Aidha amesema mwelekeo wa serikali ni kuwatia moyo wazalishaji wakubwa wa samaki ili uwekezaji uwe na tija kwa taifa kwa kupatikana kwa chakula na ajira kwa nchi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari alivyoambatana navyo kukagua shamba la fugaji samaki linalomilikiwa na Kampuni ya Tanlapia lililopo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani na kubainisha kuwa serikali itahakikisha inaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji katika sekta ya uvuvi ili kuongeza uzalishaji wa samaki nchini pamoja na ajira. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Amesema kupitia shamba la Tanlapia ambalo katika awamu ya kwanza linatarajia kuwa na mabwawa 48 ya samaki, kuwa shamba darasa la watu kutoka maeneo mbalimbali nchini kujifunza namna ya ufugaji wa samaki kibiashara.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madala, amesema teknolojia inayotumika kwenye ufugaji samaki katika shamba la Tanlapia unaweza kufuga samaki wengi kwa kuwa ina mfumo wa kusafisha maji hayo na kuwa na uwezo wa kufuga samaki wengi kwa wakati mmoja na kufungua fursa ya kufuga samaki wengi katika eneo dogo.

Ameongeza kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza kusini mwa janga la sahara kutumia teknolojia hiyo na kwamba watanzania wengi wanaweza kujifunza katika kuongeza tija ya uzalishaji wa samaki kwenye mabwawa hayo na kufafanua kuwa idadi ya watu imekuwa ikiongezeka lakini maziwa na Bahari ya Hindi haviongezeki hivyo lazima kuwa na mbinu ya kuongeza samaki kupitia njia ya ufugaji kwa kuwa duniani wastani wa kila mtu anatakiwa kula Kilogramu 20.5 kwa mwaka lakini kwa Tanzania wastani kwa sasa kwa mtu anakula Kilogramu 8.5 pekee.

Muonekano wa baadhi ya mabwawa ya kufugia samaki yanayomilikiwa na Kampuni ya Tanlapia yaliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo mradi huo una lengo la kuzalisha takriban vifaranga Milioni Mbili kwa mwaka na kuuza samaki metriki tani 8,000 hadi 10,000 kwa mwaka, kampuni imekuwa ikihakikisha inatoa ushirikiano kwa majirani ili nao pia waweze kupata elimu ya ufugaji samaki ili kuongeza tija kwao na taifa kwa ujumla na kwamba mradi utaajiri wafanyakazi 200. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanlapia inayomiliki shamba la kufuga samaki aina ya sato katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani, Bw. Baraka Karangahe amesema lengo la mradi ni soko la hapa nchini ili kila mwananchi aweze kupata samaki kwa bei nafuu na kuishukuru serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano kwa wawekezaji hapa nchini.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo ambao utakuwa unazalisha takriban vifaranga Milioni Mbili kwa mwaka na kuuza samaki metriki tani 8,000 hadi 10,000 kwa mwaka, kampuni imekuwa ikihakikisha inatoa ushirikiano kwa majirani ili nao pia waweze kupata elimu ya ufugaji samaki ili kuongeza tija kwao na taifa kwa ujumla na kwamba mradi utaajiri wafanyakazi 200.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *