Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo leo tarehe 05 October, 2021 amefanya ziara maalumu ya kumtembelea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi Ikulu Zanzibar.
Katika ziara hiyo ya kikazi iligusia mafanikio makubwa yaliyo patikana ndani ya kipindi kifupi kwa shughulikia Hoja kumi na moja za Muungano pamoja na kazi kubwa inayo endelea ya kumalizia Hoja 7 za muungano zilizobaki.
Jambo lingine kubwa lililo wasilishwa na Waziri Jafo ni suala la Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo kilichopo Jijini Dodoma kuweza kufungua tawi la chuo hicho mjini Zanzibar ili kuwawezesha watendaji, wanafunzi, na madiwani kupata fursa ya mafunzo yaliyobobea katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa.
Katika kikao hicho waziri Jafo alimshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa msaada mkubwa anaowapatia katika kutimiza majukumu aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kushughulikia masuala ya Muungano.
Pia amemshukuru Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Khalid Mohammed kwa ushirikiano mkubwa wa kushughulikia kwa pamoja hoja mbalimbali za muungano.
Aidha, Jafo amewashukuru na kuwapongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa imani yao juu yake na kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuimarisha Muungano na kuwaletea maendeleo wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiweko wananchi wa Ugunja na Pemba.
Kwa upande wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amempongeza Waziri Jafo na Dkt. Khalid Salumu Mohammedi- Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais – Zanzibar kwa ushirikiano wao mkubwa na kuchapakazi kwa kasi na kuwezesha kuondoa hoja 11 za Muungano kati ya hoja 18 zilizokuwa bado hazijapata ufumbuzi hapo awali.
Mhe. Rais Dkt. Hussein Mwinyi amepongeza pia juhudi kubwa zinazofanywa kwa upande wa Mazingira. Pia Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amefurahishwa na amekubali suala la Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo kuja kufungua tawi mjini Zanzibar kwani kitasaidia kujenga viongozi na wataalamu katika masuala ya Serikali za Mitaa.
Licha ya pongezi, Dkt. Hussein Mwinyi ameelekeza na kusisitiza kuendeleza kasi katika kushughulikia hoja zilizobaki za Muungano na Ushirikiano katika kushughulikia masuala ya mazingira.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri Mwenyeji Dkt. Khalid Mohammedi – Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza wa Wawakilishi, Bi. Mary Maganga Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais-SMT, Bw. Mohammed Abdullah, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais – SMT, na Kaimu Mkurugenzi wa Muungano Bi. Cesilia Nkwamu