RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUTEKELEZA MRADI WA LNG – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kwa dhati kuhakikisha kuwa mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) utakaogharimu Dola za Kimarekani bilioni 30 sawa na takriban shilingi trilioni 70, unaanza kazi ili kuleta manufaa kwa wananchi.

Majaliwa ameyasema hayo (Jumanne, Oktoba 5, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Likong’o wilayani Lindi baada ya kukagua eneo la ujenzi wa mradi wa LNG akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa wa Lindi.

Ad

Amesema kwa sasa mradi huo umefikia katika hatua ya majadiliano ya kimkataba na wawekezaji wa mradi huo, hivyo amewataka waliochukua viwanja karibu na eneo la mradi waanzeni kuvijenga kwani baada ya kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na watu wengi watakaohitaji makazi.

“Mradi huu unakuja na fursa nyingi za kimaendeleo, zikiwemo ajira kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka eneo la mradi pamoja na Watanzania kwa ujumla hivyo tujitahidi kuwa walinzi wa eneo hili lisivamiwe. Mheshimiwa Rais Samia amepania kuutekeleza katika awamu hii ya sita.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio amesema wakazi zaidi 600 wa mitaa ya Likong’o na Mto Mkavu katika Manispaa ya Lindi wameshalipwa shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya kupisha mradi wa LNG. Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 2071.

Dkt. Mataragio amesema Oktoba 20 mwaka huu Serikali ya Tanzania kupitia TPDC inatarajia kufanya majadiliano na wawekezaji kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo. Aliongeza kuwa kwa sasa waendelea na uwekaji wa alama zinazoonekana kuzunguka eneo lote la mradi ili liweze kutambuliwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo nchini, hivyo amewataka wananchi wafanye maandalizi ya kufikisha nishati hiyo katika makazi yao.

Alisema Rais Samia anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme nchi nzima ikiwemo na vijiji vya wilaya ya Lindi. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.

Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nyaya, nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *