DKT. BITEKO AWATAKA WAFANYABIASHARA WA MADINI KUSAJILI MIKATABA NA WABIA WAO TUME YA MADINI

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza na wafanyabiashara wa madini katika Soko Kuu la Dhahabu Mkoani Geita leo Oktoba 6, 2021. (Picha na Steven Nyamiti-WM).

Na Steven Nyamiti- WM

Wafanyabiashara wa madini wametakiwa kuingia mikataba na wabia wao kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha mikataba hiyo inasajiliwa katika ofisi ya Tume ya Madini ili itambuliwe na Serikali.

Ad

Rai hiyo imetolewa leo Oktoba 6, 2021 na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko alipotembelea na kuzungumza na Wafanyabiashara Wakubwa na wadogo wa Madini (Dealers & Brokers) katika Soko Kuu la Madini ya Dhahabu mkoani Geita.

Dkt. Biteko ameagiza ubia wa wafanyabiashara wa madini na wawekezaji usajiliwe kwenye ofisi za Serikali ili itambulike kisheria na kusaidia kutatua migogoro inapojitokeza kwa kudhulumiana au kupoteza uaminifu.

Wafanyabiashara wa madini wakimsikiliza Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko leo Oktoba 6, 2021 mkoani Geita.(Picha na Steven Nyamiti-WM).

Amesema, wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo wanatakiwa kuifanya kazi yao ipasavyo na kusimamia madini yasitoroshwe. Pia, kulipa kodi na tozo stahiki za Serikali hivyo kuwafanya watendaji kuweka nguvu kubwa katika kusimamia shughuli za madini.

Akizungumzia kuhusu uongezaji thamani madini, Dkt. Biteko amesema kuwa, Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameelekeza uongezaji thamani wa madini ufanyike hapa hapa nchini ili kulinda ajira za Watanzania na kuepusha Tanzania kuwa chanzo cha malighafi ya viwanda ya nchi za wenzetu.

Mwenyekiti wa Soko la Madini Mkoa wa Geita,Situmaini Bigazaba akizungumza wakati wa ziara ya Waziri Dkt. Biteko alipokutana na wafanyabiashara wa madini katika Soko Kuu la Dhahabu mkoani Geita leo Oktoba 6, 2021.(Picha na Steven Nyamiti-WM).

“Kuanzia madini ya Vito, madini ya Dhahabu, hatumpi mtu leseni ya ‘Dealer’ mpaka awe na mashine 30 za kukata madini ili madini hayo yaongezwe thamani hapa ndani na si kusafilisha madini ghafi,” amesisitiza Dkt. Biteko.

“Tuliamua kujenga viwanda vya kusafisha madini ili tusafishe madini ndani ya nchi. Hatuwezi kuwa na viwanda hapa halafu mtu akabeba madini akapeleka Uswisi kwenda kusafisha wakati hapa tunasafisha na viwanda vipo,” ameeleza Dkt. Biteko.

Aidha, amesema Serikali inaunga mkono biashara na shughuli za madini ili wafanyabiashara na wawekezaji wafanye vizuri zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Madini Geita, Situmaini Bigazaba ameipongeza Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Geita kwa kusimamia biashara ya madini na kutoa maelekezo mbalimbali ya taratibu za biashara ikiwemo Kanuni na Sheria zinazowalinda wafanyabiashara wa madini.

Waziri Dkt. Biteko amefanya ziara ya siku moja mkoani Geita ambapo amekutana na wadau mbalimbali wa madini kuzungumza nao na kutatua migogoro katika shughuli zao.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *