Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 21 Machi 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Austria Balozi Celestine Mushy,mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais amempongeza Balozi huyo kwa kuteuliwa na imani aliopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuliwakilisha taifa nchini Austria. Amemsihi Balozi huyo kwenda kufanya kazi kwa weledi na uzalendo kwa maslahi ya taifa.
Aidha amemtaka Balozi huyo kutambua vipaumbele vya taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu takwimu za msingi ikiwemo Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, Dira ya taifa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na fursa zinazopatikana nchini zitakazochagiza katika kutafuta wawekezaji.
Amesema ni muhimu kwa Balozi huyo kufanya jitihada za makusudi kuifahamu vema nchi anayokwenda kuiwakilisha Tanzania ili kuweza kujifunza misingi ya ukuzaji wa uchumi wao na kuhamisha maarifa hayo kwa taifa la Tanzania.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi hivyo amemuagiza Balozi huyo kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania. Aidha amemtaka Kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini pamoja na kutafuta fursa mbalimbali kwa nchi ya Tanzania ikiwemo kuwavutia watalii na kutafuta fursa za lugha ya Kiswahili ikiwemo ufundishaji na ukalimani.
Aidha amesema Balozi huyo anapaswa kuwaunganisha watanzania wanaoishi katika nchi ya Austria ili kuwa na mawazo ya pamoja namna wanavyoweza kuwekeza hapa nchini na kurudisha ujuzi na maarifa walioyonayo nyumbani Tanzania.
Makamu wa Rais ametaka Balozi Mushy kuwa na nidhamu ya matumizi ya pesa zinazopelekwa katika kuendesha Ubalozi ili kuongeza tija ya uwakilishi katika nchi hiyo.
Kwa Upande wake Balozi Celestine Mushy amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliompa na kumuahidi Makamu wa Rais kwenda kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, weledi na maarifa katika kuiwakilisha Tanzania nchini Austria. Amesema atazingatia vipaumbele vyote vya taifa na kutimiza kazi zake kwa vitendo.