KWA MARA YA KWANZA WATAALAMU WAZAWA WAZIBUA MISHIPA PACHA YA MOYO ILIYOZIBA KWA ASILIMIA 95

Kwa mara ya kwanza wataalamu wazawa wa magonjwa ya moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamezibua mishipa miwili iliyokuwa inapeleka damu kwa wakati mmoja kwenye moyo (mishipa pacha ya damu – bifurcation lesion) ambayo ilikuwa imeziba kwa asilimia 95 na kupata shida ya kupitisha damu.

Uzibuaji wa mishipa hiyo ulifanyika kwa njia ya upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum Invasive Surgery) bila kufungua kifua kwa kutoboa mshipa kwenye paja (Percutaneous Coronary Angioplasty) kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa ajili ya uchunguzi na tiba za magonjwa ya moyo.

Ad

Hayo yamesemwa hivi karibuni  jijini Dar es Salaam na daktari mbobezi wa magonjwa ya moyo Tulizo Shemu ambaye pia ni mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kumaliza kufanya upasuaji huo uliochukuwa masaa mawili na nusu na kuhusisha jopo la madaktari wabobezi watatu.

Dkt.Shemu alisema uzibuajia wa mishipa miwili pacha ambayo imeziba kwa wakati mmoja walikuwa wanafanya kwa kushirikiana na wataalamu wenzao kutoka nje ya nchi ambao wanafika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu na mafunzo lakini sasa hivi wataalamu wazawa wameweza kufanya wenyewe upasuaji wa aina hiyo.

Alisema kabla ya kufanya upasuaji huo walikuwa wanakutana na wagonjwa ambao mishipa kama hiyo ilikuwa imeziba, walikuwa wanazibua upande mmoja wa mshipa wa moyo na baada ya siku kadhaa kupita wanazibua mshipa mwingine uliobaki jambo ambalo lilikuwa linaweza kusababisha mshipa uliozibuliwa nao kuziba tena na kuhatarisha maisha ya mgonjwa. Pia kufanya gharama ya upasuaji kuwa  mara mbili kwa mgonjwa.

 “Wakati wa kufanya uchunguzi tuligundua mishipa hii muhimu ya damu ilikuwa imeziba kwa wakati mmoja tumefanikiwa kuizibua yote miwili. Kufanya upasuaji wa aina hii siyo rahisi kwani ni upasuaji mgumu (Complex Percutaneous Coronary Intervention – PCI), katika upasuaji  huu wataalamu wanakuwa wengi, vifaa vinavyotumika ni vingi na vya aina tofauti tofauti na  tunatumia muda mrefu.Faida za kufanya upasuaji wa kuzibua mishipa miwili kwa pamoja  ni kuokoa maisha ya mgonjwa na kuokoa gharama za upasuaji”, alisema Dkt. Shemu.

Alisema mishipa ya damu ya  moyo inaziba kutokana na kuwepo kwa mafuta mengi katika mishipa (cholesterol) hiyo ambayo inapatikana kwa kula kiasi kikubwa cha  vyakula vyenye  wanga, sukari  na vyenye mafuta mengi kwani katika mwili wa binadamu mafuta  yanahifadhiwa sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye ini, figo, moyo na mishipa ya damu.

Dkt. Shemu alisema magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo yamekuwa yakisababisha vifo vya ghafla na kiharusi na kuwataka watu wanapojisikia moyo kuuma, mwili kuchoka baada ya kufanya kazi kidogo au kutembea umbali mfupi kuwahi hospitali mapema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kama watakutwa na matatizo ya moyo waweze kupata matibabu mapema na kwa wakati wakikaa nyumbani shida zitaongezeka zaidi pamoja na kupoteza maisha.

“Sasa hivi magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo  yanasababisha vifo vya watu wengi ni muhimu kubadili mtindo wa maisha kwa kula chakula bora, kufanya mazoezi, kunywa pombe kwa kiasi, kuacha kuvuta sigara na kupunguza  msongo wa mawazo wanaokutana nao katika maisha kwa kufanya hivyo unaweza kuepuka kupata magonjwa haya”, alisisitiza Dkt. Shemu.

Kwa upande wake Mama Sada Haji kutoka Zanzibr ambaye alizibuliwa mishipa hiyo ya damu alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema alikuwa anapata maumivu makali eneo la kifuani upande  wa kushoto, akibeba mizigo mdogo anakosa nguvu pia anatoka jasho jingi.

“Baada ya kujisikia maumivu nilipelekwa Hospitali ya kwanza na kuandikiwa dawa za kutumia nilizitumia dawa hizo kwa muda wa miaka nane lakini tatizo likawa linaendelea. Watoto wangu walinipeleka  Hospitali nyingine na kufanyiwa vipimo na kugundulika kuwa na tatizo kwenye moyo daktari akanituma kuja kutibiwa hapa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. Baada ya kufika hapa na kufanyiwa vipimo siku ya Alhamisi iliyopita niliambiwa mishipa miwili ya damu ilikuwa imeziba na inatakiwa kuzibuliwa”,.

“Siku ya Jumatatu tarehe 4/04/2022 nilifanyiwa upasuaji wa kuzibuliwa mishipa hiyo baada ya kufanyiwa upasuaji huo sasa hivi najisikia vizuri, maumivu hakuna tena kama ilivyokuwa awali, ninakula chakula vizuri na daktari ameniambia nitaruhusiwa kurudi nyumbani siku chache zijazo”, alisema Mama Sada.

Mama Sada aliwashauri watu wenye matatizo kama yake wasikate tamaa wakisikia maumivu waende Hospitali wakafanyiwe uchunguzi kwani vifaa vipo na wataalamu wapo wanaotoa huduma za kuzibua mishipa ya damu ya moyo.

                                                                                                                   

Ad

Unaweza kuangalia pia

#LIVEDAY2: JUKWAA LA KODI NA UWEKEZAJI 2024

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.