Kongamano la Wadau wa Mazingira – (NEMC) 31 Mei 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameagiza kuangaliwa upya kwa sheria zinazohusu uhifadhi wa mazingira ili kuliwezesha Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Halmashauri kuwa na nguvu ya kuchukua hatua kali dhidi ya uharibifu wa Mazingira.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam. Amesema uchafuzi wa mazingira katika Majiji, Miji na Halmashauri bado ni tatizo huku uharibifu wa misitu ukiendelea kuwa changamoto licha ya kuwepo kwa vyombo vya kuishauri Serikali juu ya masuala ya utunzaji wa misitu na mazingira pamoja na kuwepo kwa Sheria ndogo katika ngazi ya Serikali za mitaa.

Ad

Aidha Makamu wa Rais amewasihi Watanzania kuacha mazoea ya kukata miti na kutupa taka hovyo na kuziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe kuwa Kampuni zinazopewa kazi ya kuzoa taka ziwe na uwezo wa kufanya kazi hizo kwa ufanisi.

Vilevile Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhimiza wataalamu katika vyuo hapa nchini na taasisi za utafiti kufanya utafiti mahususi kwa ajili ya kupambana na kuenea kwa jangwa kwa kutumia teknolojia na ubunifu. Ameutaka uongozi wa mikoa inayokabiliwa na kuenea kwa jangwa ikiwa ni pamoja na Halmashauri kuchukua hatua za ziada kupanda miti pamoja na mazao yanayostahimili ukame kama mitende.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa Watendaji wote wa Wizara, Wakuu wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wengine, kuhamasisha na kutoa elimu kwa Wananchi juu ya utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Amesema ni vema kuelimisha umma kuachana na mila potofu zinazoharibu misitu, vyanzo vya maji na uoto wa asili na kuhimiza matumizi ya Nishati safi ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa rai ya matumizi ya lugha ya kiswahili katika machapisho yote ya utunzaji wa mazingira ili walengwa ambao ni wananchi wa Tanzania waweze kuelewa juu ya masuala ya mazingira kirahisi.

Ad

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *