Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha, kuvutia na kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya madini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia ametenga kiasi cha shilingi bilioni 118 kwa ajili ya kupeleka umeme kwa wachimbaji madini na kwa upande wa Kanda ya Ziwa kuna maeneo zaidi ya 90 ambayo yanatarajiwa kupelekewa umeme.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2024 mkoani Geita wakati akifungua Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini.
“ Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru tena Watanzania wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kuendeleza sekta mbalimbali za kiuchumi. Wajibu wa Serikali ni kuendeleza jitihada za kujenga na kuimarisha misingi thabiti ya uchumi katika kuvutia wawekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini, amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa lengo la Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ni kuhakikisha sekta hiyo inafungamanishwa na sekta nyingine za kiuchumi ili kuleta tija na maendeleo ya haraka kwa watu hasa kupitia ajira mbalimbali zinazotokana na shughuli za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara ya madini nchini.
“ Ili sekta ya madini iweze kuongeza mchango wake kwenye uchumi wa nchi ni lazima ifungamanishwe kikamilifu na sekta muhimu za uchumi. Ufungamanishaji wa sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi ni dhahiri kuwa utaliletea Taifa maendeleo kwa haraka kwa kuwezesha upatikanaji wa ajira pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.” Amesema Dkt. Biteko.
Aidha, ametoa rai kwa Watanzania kujituma, kubadilisha mtizamo na kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea jitihada za Serikali za kuinua uchumi wa nchi.
Pia, Dkt. Biteko ameipongeza Wizara ya Madini kwa jitihada zake za kuanzisha uwepo wa akiba ya dhahabu, sambamba na kuipongeza Benki Kuu ya Tanzania.
Akizungumzia kaulimbiu ya maonesho hayo ya madini kwa mwaka 2024 yenye ujumbe usemao “Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Nishati Safi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Endelevu”.
Dkt. Biteko amesema kuwa matumizi ya teknolojia na nishati safi katika shughuli mbalimbali ikiwemo shughuli za madini hususan katika utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani madini ni muhimu na hayaepukiki.
“ Katika kufanikisha hili matumizi sahihi ya teknolojia ni muhimu sana ili kufanya shughuli za uchimbaji hasa zinazofanywa na wachimbaji wadogo zifanyike kwa kuzingatia vifaa na teknolojia ya kisasa ili kufanya uchimbaji wao uwe na tija na unaozingatia utunzaji wa mazingira.” Amesisiza Dkt. Biteko.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa kwa sasa bajeti ya wizara yake ni shilingi bilioni 232 kutoka shilingi bilioni 90 iliyokuwa awali ambapo wamejiandaa kujenga maabara kubwa ya kisasa ili wachimbaji wapate fursa ya kufanya utafiti wa madini badala ya kwenda nje ya nchi
“ Haya tunayafanya chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia na ambaye ameelekeza kununua mitambo 15 ya uchimbaji madini ambayo tutaigawa nchi nzima ikiwemo kwa vikundi vya uchimbaji vya akina mama na vijana.” Amesema Mhe. Mavunde.
Ameongeza kuwa mwaka 2017 sekta hiyo ilichangia asilimia 7.1 katika Pato la Taifa na sasa inachangia kwa asilimia 9.0 huku malengo ikiwa ni asilimia 10 ifikapo 2025.
Amefafanua “ Naamini ikifika mwakani tutafikia lengo kwa kuwa vipo viashiria vinavyoonesha jambo hili linawezekana na malengo yetu kwa mwaka huu wa fedha tutachangia shilingi trilioni 1 katika Mfuko Mkuu wa Serikali.”