Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Biashara na Uchumi kati ya Tanzania na Urusi, uliofanyika jijini Dar es Salaam, umehitimishwa kwa mafanikio kwa kusainiwa kwa vipengele mbalimbali vya makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Mkutano huo wa siku mbili ulijumuisha mkutano wa wataalamu, mkutano wa Tume ya Pamoja, na kongamano la uwekezaji. Makubaliano haya yalitiwa saini kwa ngazi ya mawaziri na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo kwa upande wa Tanzania, na Waziri wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Urusi, Mhe. Maxim Reshetnikov.
Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alibainisha kuwa Tanzania na Urusi zimekuwa na uhusiano wa miaka sitini uliowekwa imara katika sekta za siasa na utamaduni, huku ukileta manufaa makubwa katika elimu, sayansi, na teknolojia. Amesema kuwa makubaliano haya mapya yanapanua wigo wa ushirikiano katika sekta muhimu kama viwanda, biashara, fedha, nishati, kilimo, uchukuzi, afya, habari na mawasiliano, na teknolojia ya habari. Aidha, maeneo ya maliasili, utalii, utamaduni, na michezo yamejumuishwa pia.
Kwa upande wake, Waziri Reshetnikov amepongeza juhudi za Tanzania katika kuimarisha uchumi wake, na kusema kuwa Urusi inalenga kuifanya Tanzania kuwa mshirika wa kimkakati wa masuala ya biashara na uchumi barani Afrika.
Pia, mkutano ulihudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Pindi Chana, Naibu Waziri wa Viwanda Mhe. Exaud Kigahe, na Mhe. Injinia Meryprisca Mahundi.