????????????????????????????????????

MABULA AKAGUA MIRADI YA SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC) WILAYANI CHATO MKOANI GEITA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika moja ya nyumba za watumishi wa hospitali ya rufaa ya Kanda- Chato wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wilayani Chato mkoani Geita tarehe 14 Septemba 202. 
 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekagua miradi ya shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wilayani Chato mkoani Geita na kusikitishwa na kusuasua kwa utekelezaji wake kunakosababishwa na ucheleweshaji wa fedha.

Dkt Mabula alikagua miradi mitatu inayotekelezwa na NHC ambayo ni mradi wa mnada wa mifugo Buzirayombo wenye thamani ya shilingi Bilioni 4.8, mradi wa ujenzi wa shule maalum ya Mbuye Bilioni 5.14 pamoja na mradi wa nyumba 20 za watumishi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato wa thamani ya shilingi Bilioni 1.139

Ad

Akizungumza mara baada ya kukagua miradi yote mitatu leo tarehe 14 Septemba 2021 wilayani Chato mkoani Geita akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo, Dkt Mabula alisema, miradi hiyo ni muhimu na inapaswa kukamilika kwa wakati ili ianze kutumika.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozwa na Mkuu wa wilaya ya Chato mkoani Geita Martha Mkupasi (Kushoto) kukagua ujenzi wa mradi wa shule maalum Mbuye unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wilayani Chato tarehe 14 Septemba 202.

“Haitakuwa na maana Serikali kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi wa mnada wa mifugo, shule maalum na nyumba za watumishi wa sekta ya afya na kuachwa bila kukamilika jambo ambalo halitaleta maana”. alisema Dkt Mabula.

Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera Maneno Mahenge alimwambia Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa shirika lake la NHC limekuwa likisuasua kutekeleza kwa kasi miradi katika wilaya hiyo kutokana na kutopatiwa fedha za miradi kwa wakati.

Kwa mujibu wa Meneja wa NHC mkoa wa Kagera,  Shirika lake hadi kufikia sasa limetumia takriban bilioni 1.02 kwenye mradi wa mnada wa mifugo,  milioni 985 katika shule maalum ya Mbuye na milioni 275 kwa ajili ya utekelezaji mradi wa nyumba za watumishi katika hospitali ya Rufaa ya Kanda na fedha zote hizo bado hawajalipwa.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati akikagua ujenzi wa mradi wa mnada wa mifugo unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wilayani Chato mkoani Geita tarehe 14 Septemba 202. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Chato Martha Mkupasi na kushoto ni Meneja wa NHC Kagera Maneno Mahenge.

Naibu Waziri Dkt Mabula alisema, pale panapokuwa na changamoto yoyote katika utekelezaji miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa basi ni lazima ushirikiano uwepo baina ya mwenye mradi na mkandarasi kwa lengo la kuepuka ucheleweshaji.

“Kama taarifa hazifiki kwa wakati basi miradi itasimama na haileti picha nzuri na ukiangalia hapa tatizo kubwa ni mawasiliano na taarifa zikiwepo basi kazi itaenda vizuri” alisema Dkt Mabula. 

Dkt Mabula aliahidi kukutana na wenye miradi ili aweze kusukuma miradi hiyo iweze kukamilika haraka na kuanza kutumika.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, zoezi la uhakiki kwa wamiliki wa ardhi nchini halina lengo la kuwanyang’anya umiliki wa ardhi maeneo yao bali ni kutaka kutambua wamiliki kwa majina.

Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi na viongozi wa wilaya ya Chato mkoani Geita Dkt Mabula alisema, kuna baadhi ya viwanja wamiliki wake hawajulikani na zoezi la uhakiki linaloendelea sasa nchini linataka kumtambua na kuanisha kila mmiliki na eneo lake.

“Kuna viwanja vimepimwa zamani na wamiliki wake hawaonekani tunataka kujua wamiliki ni kiasi gani na tunahitaji uhakiki kuwatambua watanzania kupitia utajiri wao kwenye sekta ya ardhi” alisema Dkt Mabula

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA MRADI WA MAJI SAME MWANGA KOROGWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji Maji wa Same – Mwanga – Korogwe wakati alipotembelea chanzo cha mradi huo eneo la la Nyumba yaMungu Wilaya ya Mwanga wakati akiwa ziarani mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024. Makamu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *