TANZANIA KINARA MASUALA YA MAAFA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kusaini mkataba wa kuanzisha Kituo cha Huduma za Binadamu na Operesheni za Dharura cha Kanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). “Lengo la kuanzisha kituo hicho ni kusimamia utoaji wa huduma na misaada ya kibinadamu kwa nchi wanachama. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, masuala ya majanga hayana mipaka na hayana muda na yanahitaji jitihada za pamoja katika kuyashughulikia,” amesema. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 5, 2023) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024. “Kama mtakumbuka, katika kuendeleza uhusiano na nchi nyingine, hivi karibuni nchi yetu imeungana na mataifa mengine duniani kutoa misaada ya kibinadamu kwa nchi zilizopatwa na maafa makubwa yaliyosababisha vifo na majeruhi, uharibifu wa mali na mazingira. Nchi hizo ni Malawi iliyokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Freddy kilichotokea tarehe 13 Machi, 2023 na Uturuki iliyokumbwa na tetemeko la ardhi Februari, mwaka huu,” amesema. Ameitaja misaada iliyotolewa Malawi kuwa ni tani 1,000 za mahindi, mablanketi 6,000, mahema 50, fedha taslimu sh. milioni 705, dawa za binadamu na helikopta mbili kwa ajili ya kusaidia uokoaji. Vilevile, Uturuki ilipewa dola za Marekani milioni moja. Akielezea utekelezaji wa shughuli za maafa kwa mwaka 2022/2023, Waziri Mkuu Majaliwa amesema wajumbe 555 wa Kamati za Usimamizi wa Maafa na Waratibu wa Maafa walipatiwa mafunzo ya kuimarisha uwezo wa utendaji kazi katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara na Singida. “Pia wavuvi 344 katika mwambao wa Ziwa Victoria na vijana 40 wa kujitolea katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Songwe na Tabora walipata mafunzo ya uokoaji, yaliyowaongezea uwezo wa kukabiliana na maafa kwa wakati,” amesema.

Ad

Unaweza kuangalia pia

“Tukamate wajibu wetu tuliopewa na Mungu, wa Kukuza watoto wetu katika maadili mema”.‪@samiasuluhu99‬

Twende tukatunze Watoto wetu vile sisi tulivyotunzwa na Wazazi Wetu katika maadili mema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *