Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, kusimamia kikamilifu Sheria ya Usajili wa Jumuiya pamoja na kanuni zake ili kuhakikisha kuwa Taasisi zinazosajiliwa zikiwemo za kidini zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo na masharti ya usajili wake.
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach iliyofanyika katika kanisa hilo Sakina mkoani Arusha. Amesema hivi sasa yameibuka mafundisho ya baadhi ya viongozi wa dini yanayowaaminisha wafuasi wao kutegemea miujiza zaidi ili kupata maendeleo badala ya kufanya kazi kwa bidii.
Ameongeza kwamba imeshuhudiwa kuongezeka kwa wahubiri wanaojilimbikizia fedha na mali binafsi kutokana na sadaka na mauzo ya vitu mbalimbali na wengi wa wahanga wa mahubiri ya aina hiyo ni wananchi wanaokabiliwa na shida au matatizo mbalimbali ya maisha.
Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini kuungana na serikali kukemea vikali mafundisho na matendo hayo yasiyofaa katika jamii na yasiyozingatia sheria za nchi. Pia ametoa wito kwa viongozi wote kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uzalendo, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu abariki kazi zao.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema hivi sasa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii hali inayopelekewa na matumizi holela ya mitandao ya kijamii, ambapo wananchi hususan vijana wengi wanadhani ili kuwa kijana wa kisasa, inawalazimu kuiga mambo yanayooneshwa kwenye mitandao hiyo yakiwemo yale yasiyo endana na mila na desturi.
Amesema kukosekana kwa hofu ya Mungu katika jamii kunapelekea kuongezeka kwa matukio ya mauaji ya kikatili, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na wanawake, familia za mzazi mmoja, watoto waliozaliwa nje ya ndoa, migogoro ya ndoa, talaka, migogoro ya mirathi na ardhi, ubadhirifu wa mali za umma na matukio ya watu kujinyonga.
Aidha Makamu wa Rais amekemea tabia za uzembe na kutozingatia sheria za usalama barabarani ambazo zimepelekea kushamiri kwa ajali mbaya za barabarani zinazogharimu maisha ya wananchi wengi.
Ametoa rai kwa wakaguzi wa magari wa LATRA na Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani kutimiza wajibu wao ili kudhibiti magari mabovu yasiingie barabarani na kuhakikisha vidhibiti mwendo vinafanya kazi, pamoja na kukagua sifa za madereva hasa wa mabasi ya abiria na malori. Ameongeza kwamba wamiliki wa Mabasi na Malori wanapaswa kuhakikisha magari yao yanakuwa na madereva walau 2 kwa safari zote ndefu zinazozidi kilomita 300. Vilevile ameagiza Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha alama za tahadhari zinawekwa katika maeneo yote hatarishi ya barabara kuu.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa wasafiri wote nchini kuzingatia kufunga mikanda wakati wote wa safari na kutoa taarifa kwa Kikosi cha Usalama Barabarani pale dereva wa chombo wanachosafiria anapoendesha kwa mwendo mkali kupita kiasi.
Pia Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kushirikiana na serikali katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Amesema uhai wa wanadamu katika dunia unatishiwa na uharibifu wa mazingira ambao umekithiri ambapo pamoja na jitihada mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazochukuliwa kukabiliana na hali hiyo, lakini bado matokeo yake si ya kuridhisha. Ameongeza kwamba uharibifu wa misitu na ukataji wa miti unaonekana katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo mkoani Arusha.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuenzi mchango mkubwa wa madhehebu ya Dini, katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na itaendelea kusimamia na kulinda haki ya kuabudu kwa wananchi wote kwa mujibu wa ibara ya 19 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba wananchi wanaendelea kuishi katika mazingira ya haki na amani.