Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa misingi inayoshajihisha uongozi wake ni ufanyaji wa maamuzi kwa kushirikisha wadau, kwa kuoongozwa na ushahidi na utafiti, na kwa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa na Watanzania.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati akitunikiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Uongozi na Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Morogoro kwenye Sherehe ya Mahafali ya 23 ya Chuo hicho.
Itakumbukwa kuwa Rais Dkt. Samia alisoma katika Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 1983 hadi 1986, na sasa amekuwa mtunukiwa wa kwanza wa heshima hiyo katika Chuo hicho.
Rais Dkt. Samia ameeleza namna misingi ya uongozi wake katika kufanya maamuzi ilivyoiwezesha Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokabili nchi ndani ya miaka mitatu ya Awamu ya 6, ikiwemo athari za mlipuko wa UVIKO-19 na migogoro ya kimataifa ambayo ziliathiri mwenendo wa uchumi wa dunia.
Rais Dkt. Samia ametumia fursa hiyo pia kutambua na kupongeza michango ya Awamu za uongozi zilizotangulia iliyoliwezesha Taifa kuwa lenye utawala bora, utulivu wa kisiasa, uchumi imara, amani na mshikamano.
Pamoja na kusisitiza kuwa kiongozi ni mtumishi anayeendeleza ya jana, anayebuni, kuibua na kutekeleza ya leo na anayeacha ya kuendelezwa kwa ajili ya kesho, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa viongozi wote kwa nafasi zao kufanya kazi na kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia maadili na uadilifu.
Akizungumzia elimu ya juu, Rais Dkt. Samia amesema kuwa Serikali itaongeza uwekezaji katika teknolojia, tafiti zenye manufaa na mipango kwa lengo la kuimarisha elimu ya juu na kuwezesha wahitimu kuwa na ushindani kikanda na kimataifa.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amerejea rai yake kwa vyuo vikuu nchini kujielekeza katika kujibu changamoto za mazingira ya sasa, kitaifa, kikanda na kimataifa.