Amesema mpango huo umejikita katika kuendeleza na kukamilisha utekelezaji wa afua zinazotoa matokeo ya maeneo matano ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 8, 2024) wakati akiahirisha Mkutano wa 17 wa Bunge la 12 Bungeni jijini Dodoma, ambapo amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026.
“Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi itaweka mkazo katika maeneo ya miradi ya kielelezo yenye manufaa na matokeo makubwa na kujielekeza katika vipaumbele vya mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026.”
Amesema vipaumbele hivyo ni: kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimaliwatu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kusimamia makusanyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025 ambapo jumla ya shilingi trilioni 11.55 zimekusanywa kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi. “Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 7.93 ni mapato ya ndani, sawa na asilimia 99.4 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 7.97.”
“Mapato hayo yanajumuisha mapato yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania shilingi trilioni 7.09, mapato yasiyo ya kodi yaliyokusanywa na wizara na idara zinazojitegemea shilingi bilioni 518.32, na mapato kutoka vyanzo vya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi bilioni 321.32.”