Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema serikali imedhamiria kushirikiana na wadau, sekta binafsi pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kupambana na tatizo la taka za plastiki nchini. Amesema uzoefu unaonesha kwamba ushirikiano ni njia bora zaidi itakayowezesha kukabiliana na tatizo hilo kwani yapo maeneo ambayo taka za plastiki hutupwa na kufika katika mataifa mengine hususani kwa njia ya bahari.
Amewakaribisha Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) kupitia Ushirikiano wa Kimataifa katika Usimamizi na Menejimenti ya Taka za Plastiki kushirikiana na Tanzania katika mbinu mbalimbali za kukabiliana na uchafuzi wa taka za palstiki kama vile kuwajengea uwezo wataalamu, kuwezesha teknolojia na vifaa vya kisasa vya urejerezaji wa taka za plastiki pamoja na ufadhili wa kifedha katika miradi ya kukabiliana na uchafuzi wa taka za plastiki.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na taka za plastiki kama vile kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki pamoja na utoaji elimu ya kuhamasisha wananchi kubadili tabia ya utupaji taka za plastiki ovyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano katika Usimamizi na Menejimenti ya Taka za Plastiki wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) Bi. Clemence Schmid ameipongeza serikali ya Tanzania kwa jitihada na nia ya dhati ya kupambana na taka za plastiki.
Amesema ujumbe wa Sekretarieti ya Jukwaa la Uchumi Duniani umejionea dhamira ya dhati ya Tanzania katika kutoa kipaumbele cha juu kuzuia uchafuzi wa mazingira husasani wa taka za plastiki.
Amesema Jukwaa hilo linalenga kuanzisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania kwa lengo kuu la kuondoa taka za plastiki ambapo kupitia ushirikiano huo Tanzania inaweka mazingira rafiki ya kuongeza kushirikisha wadau wa kitaifa na kimataifa katika kuiondoa nchi kwenya adha ya taka za plastiki.
Ametaja vipaumbele katika ushirikiano huo ni pamoja na kutambua changamoto zilizopo, kuwaunganisha wadau pamoja na kutambua namna ya kutumia rasilimali fedha na uwekezaji katika kuandaa miundombinu rafiki ya kutumia vema taka za plastiki kiuchumi.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
15 Agosti 2024
Dodoma.