Makamu wa Rais Dkt. Mpango Awakaribisha Wawekezaji Katika Nishati ya Jotoardhi Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji kushirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye nishati ya Jotoardhi inayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Ametaja baadhi ya maeneo muhimu ambayo yatazalisha nishati ya jotoardhi ni pamoja na Ngozi (Megawati 60), Kyejo – Mbaka (Megawati 60), Songwe (Megawati 5-35), Natron (Megawati 60) na Luhoi (Megawati 5).

Ad

Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kwaajili ya uwekezaji katika sekta ya jotoardhi kutokana na kuwa na amani na utulivu, mazingira mazuri ya kuvutia, utulivu wa kisiasa pamoja na sera imara chini ya marekebisho ya kimuundo kupitia falsafa ya R nne za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo ni mageuzi, kujenga upya, maridhiano na ustahimilivu.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa rai kwa Nchi wanachama zenye rasilimali ya jotoardhi zinazopitiwa na bonde la ufa (ARGeo) kuwa na ushirikiano na juhudi zinazoratibiwa katika kuchunguza maeneo ya jotoardhi na kutafuta uwekezaji unaohitajika katika kutumia rasilimali hii muhimu. Amesema ni muhimu kuimarisha ubadilishanaji maarifa, mbinu bora, teknolojia pamoja na kubuni na kutekeleza programu za uchunguzi za kikanda.

Pia Makamu wa Rais amesema ni vema kwa kila nchi mwanachama   kuwa na taasisi inayosimamia na kuongoza maendeleo ya jotoardhi ikiwa ni pamoja na mifumo sahihi ya kisheria na udhibiti ambayo inaweza kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi.

Aidha amesema kutokana na bajeti za serikali kitaifa kutotosheleza kugharamia uwekezaji mkubwa unaohitajika katika awamu ya maendeleo ya miradi ya jotoardhi hivyo ni umuhimu kwa Nchi wanachama zenye rasilimali ya jotoardhi zinazopitiwa na bonde la ufa (ARGeo) kuwa na mazungumzo maalumu ya mara kwa mara na Benki za Maendeleo ya Kimataifa kama vile AfDB na Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia hivyo kufanya uwekezaji binafsi katika matumizi ya rasilimali jotoardhi kuvutia zaidi. 

Makamu wa Rais amesema Kwa sasa, Tanzania imekamilisha hatua za awali za utafiti wa rasilimali ya jotoardhi katika maeneo matano yaliyo kando ya bonde la ufa, na imeanza kuchimba visima katika moja ya maeneo yaliyopo Ziwa Ngozi upande wa Magharibi mwa ziwa hilo. Pia uchunguzi unafanywa katika miradi ya kimkakati ambayo ni Kyejo-Mbaka, Luhoi na Natron. Ametaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya Watanzania wenye utaalam wa jotoardhi na ununuzi wa mitambo ya kuchimba visima. 

Kongamano hilo la siku saba lina kauli mbiu isemayo “Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi Afrika” linashirikisha jumla ya washiriki 800 kutoka mataifa 21 duniani.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Tanzania Kuandaa Mkutano wa Kilele wa Nishati Januari 2025

Mkutano wa kilele kuhusu nishati unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa Januari 2025, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *