Rais Magufuli akutana na timu ya wataalamu wa umeme kutoka Ethiopia na timu ya Makinikia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Juni, 2017 amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Tanzania.

Mhe. Rais Magufuli amesema timu hiyo inayoongozwa na Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dkt. Seleshi Bekele imekuja nchini kubadilishana uzoefu na timu ya wataalamu wa Tanzania ambayo inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).

Ad

Katika mazungumzo na timu hiyo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli ameelezea nia yake ya kuhakikisha mawazo ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya tangu mwaka 1980 juu ya kuzalisha umeme kutoka maporomoko ya mto Rufiji, yanatekelezwa haraka iwezekanavyo.

“Sasa hivi nchi yetu inazalisha megawatts 1,450 tu, lakini Stiegler’s Gorge itatuzalishia megawatts 2,100 umeme huo ni mwingi na utatusaidia katika viwanda, hivyo Serikali tumeamua kutekeleza mradi huu.

“Najua kutaanza kutokea vipingamizi mbalimbali, lakini naomba Watanzania tuwe na sauti moja, eneo litakalotumia ni Kilometa za mraba 1,350 ambalo ni sawa na asilimia 3 tu ya eneo lote la hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 45,000” amesema Mhe. Rais Magufuli na kuongeza kuwa mradi huo utakuwa na faida nyingi zikiwemo uvuvi, maji kwa ajili ya wanyamapori na kilimo.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dkt. Seleshi Bekele amesema Ethiopia ambayo kwa sasa inazalisha megawatts 4,300 za umeme kwa kutumia maji, inayo miradi mingi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji ambayo itaiwezesha kufikia uzalishaji wa megawatts 17,000 ifikapo mwaka 2020 na kwamba yeye na watalaamu
wa nchi wapo tayari kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania Dkt. Medard Kalemani na timu ya wataalamu wa Tanzania wanaosimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na wajumbe wa kamati mbili zilizofanya uchunguzi wa madini yaliyokuwamo kwenye makontena yenye mchanga wa madini katika maeneo mbalimbali hapa nchini, na kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Mhe. Rais Magufuli amesema timu hiyo imefanya kazi nzuri na yenye maslahi makubwa kwa Taifa na kwamba Serikali itahakikisha inafanyia kazi taarifa zilizotolewa na kamati hizo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Juni, 2017

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *