Rais Magufuli ataka Jeshi la Polisi kukomesha uhalifu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi nchini kutumia weledi wake kwa kiwango cha juu katika kutekeleza jukumu lake la kulinda raia na mali zao, hasa kukomesha vitendo vya uhalifu.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 02 Juni, 2017 wakati akizungumza na Makamanda Wakuu kutoka makao makuu ya polisi, Makamanda wa Mikoa na Vikosi vya Tanzania Bara na Zanzibar na viongozi wote wakuu wa polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam waliokutana katika Bwalo la Maofisa Wakuu wa polisi lililopo Oysterbay Jijini Dar es
Salaam.

Ad

Mhe. Dkt. Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zake za kukabiliana na uhalifu lakini ametaka juhudi hizo ziongezwe hususani kukabiliana na matukio ya ujambazi na mauaji ya raia, dawa za kulevya na kuendesha operesheni zenye tija katika mikoa yote. Amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro kujipanga vizuri yeye na safu yake ya Makamanda, Viongozi Wakuu wa Vikosi na Maofisa mbalimbali ili kuondoa dosari zote za utendaji kazi zinazoshusha ufanisi na heshima ya Jeshi la Polisi.

“Ni lazima ufanye mabadiliko makubwa, nataka kuona Jeshi la Polisi linakuwa Jeshi la Polisi, Wewe IGP Sirro na Makamnda wenzako hakikisheni mnakomesha uhalifu, komesheni mauaji dhidi ya raia, ujambazi na dawa za kulevya” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Makamanda, Maofisa na Askari wa jeshi hilo kujiepusha na rushwa, dawa za kulevya, kutumiwa na watu kwa maslai binafsi, kuingia mikataba isiyo na maslai kwa Jeshi na Taifa, ubadhirifu na kuacha upendeleo katika utoaji wa ajira na vyeo.

Mhe. Rais Magufuli pia ametaka Makamanda, Maofisa na Askari wote wa Jeshi la Polisi wampe ushirikiano wa kutosha IGP Simon Sirro ambaye hivi karibuni amemteua kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini. Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Mstaafu Projest Rwegasira.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Juni, 2017

Ad

Unaweza kuangalia pia

Je! Wajua Mchango wa Madini ya Tanzanite katika Pato la Taifa?

Madini ya Tanzanite, yanayopatikana pekee katika eneo dogo la Mererani, Tanzania, ni miongoni mwa rasilimali …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *