Rais Magufuli awataka Watanzania kupuuza mjadala wa kuongeza kipindi cha Urais

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Januari, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Ndugu Polepole amesema Mhe. Dkt. Magufuli amemuelekeza kuwajulisha wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala unaoendelea juu kuongezwa kwa kipindi cha Urais kutoka miaka 5 iliyowekwa kwa mujibu wa katiba, hadi miaka 7.

Ndugu Polepole amesema Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kwa ujumla kuupuuza mjadala huo kwa kuwa haujawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha chama, na ni kinyume na katiba ya CCM na katiba ya nchi.

Ameongeza kuwa Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wana CCM na umma wa Watanzania kutokubali kuyumbishwa ama kupotoshwa na mambo yasiyokuwa ya msingi na badala yake wajielekeze katika ajenda muhimu ya kujenga uchumi na kutekeleza Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Ndugu Polepole amebainisha kuwa Mhe. Dkt. Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha Urais wakati wote wa uongozi wake.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

13 Januari, 2018

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *