Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Ali Yanga

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), uongozi wa Klabu ya Yanga na wanamichezo wote kwa ujumla kufuatia kifo cha shabiki mkubwa wa timu ya Yanga Bw. Ali Mohamed maarufu kwa jina la Ali Yanga.

Ali Yanga amefariki dunia jana tarehe 20 Juni, 2017 kwa ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Chipogolo kilichopo katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Ad

Mhe. Rais Magufuli atamkumbuka Ali Yanga kwa uzalendo wake na mchango wake wa kuhamasisha na kushabikia masuala mbalimbali ya kitaifa na hasa michezo, ikiwemo kuishabikia timu yake ya Yanga, timu ya soka ya Taifa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na shughuli za kiserikali kama vile Mwenge wa Uhuru na ziara za viongozi.

“Nimeguswa sana na kifo cha Ali Yanga, nilikuwa nae wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo alitoa mchango mkubwa katika uhamasishaji wa wananchi kukipigia kura chama changu cha CCM, na pia amekuwa akiongoza mashabiki wenzake kuishabikia timu ya Yanga na timu ya Taifa bila kuchoka. Kwa kweli alikuwa hodari sana katika ushabiki wake.

“Natoa pole nyingi sana kwa familia yake, viongozi wa timu ya Yanga, wanamichezo wote, wana CCM na wote walioguswa na kifo cha Ali Yanga na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kibaha, Pwani.
21 Juni, 2017

Ad

Unaweza kuangalia pia

WATAALAMU WA GST WAENDELEA NA UTAFITI WA MADINI PEMBA: KUKUZA MAENDELEO ENDELEVU KATIKA SEKTA YA MADINI

Katika utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Wizara ya Madini Tanzania Bara na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.