DKT.ASSEY – TUMEFANIKIWA KUBORESHA HUDUMA ZA LISHE

  • Imeelezwa kwamba katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, Taifa limefanikiwa kuimarisha huduma za lishe ikiwemo kuongeza bajeti ya lishe kuanzia ngazi ya Mikoa na Halmashauri.
  • Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Vincent Assey wakati akiongea na maafisa habari/mawasiliano na uhusiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na taasisi zake kwenye kampeni ya “Tumeboresha Afya” .
  • “Serikali imeziagiza halmashauri zote nchini kuongeza fedha zinazotengwa kugharamia huduma za lishe kutoka shilingi 500 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka 5 iliyokuwa inatengwa mwaka 2015/16 hadi shilingi 1,000 mwaka 2018/19.
  • Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Serikali imetumia shilingi bilioni 11. Hiki ni kiwango kikubwa zaidi kuwahi kutumiwa katika historia ya utoaji wa huduma za lishe hapa nchini katika kipindi cha mwaka mmoja wa fedha” alisema Dkt. Assey.
  • Pia, amesema kwamba Serikali imeendelea kuimarisha huduma ya utoaji wa vidonge vya vitamini A ya nyongeza na dawa za kutibu minyoo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5. Huduma hii inatolewa mara mbili kwa mwaka. Hadi kufikia mwezi Juni 2018 asilimia 96 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 nchini walipatiwa vidonge vya vitamini A ya nyongeza ili kuimarisha kingamwili dhidi ya magonjwa na kuboresha uwezo wa macho yao kuona vizuri
  • Aidha Dkt. Assey amesema kupitia viwanda, Serikali imefanikiwa kuboresha lishe za watanzania kwa kuviwezesha viwanda vinavyosindika vyakula kuongeza virutubishi muhimu ikiwemo Vitamini A na D kwenye mafuta ya kula, madini chuma na vitamini ya asidi ya foliki katika unga wa mahindi na unga wa ngano.
  • Vitamini A huimarisha kingamwili inayosaidia kudhibiti magonjwa mwilini, vitamini D inasaidia kuimarisha afya ya mifupa. Madini chuma yanayosaidia kuongeza wingi wa damu mwilini na vitamini ya asidi ya foliki inayosaidia pia kuongeza damu mwilini na kuzuia tatizo la watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vikubwa, mgongo wazi na midomo iliyopasuka (mdomo sungura).
  • Vilevile Serikali imewawezesha wazalisha chumvi kuongeza madini joto kwenye chumvi ili kutokomeza tatizo la upungufu wa madini joto mwilini. Kwa kudhibiti tatizo la upungufu wa madini joto mwilini Taifa linadhibiti kasi ya mimba kuharibika, watoto kufariki wakiwa tumboni, pamoja na kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na mtindio wa ubongo/taahira na ulemavu wa viungo.
  • Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe, Sikitu Saimon ameeleza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imeboresha vitendea kazi vya kutolea elimu ya lishe kwa umma kwa kutumia mfuko wa siku 1000, unaotumika katika ngazi ya jamii kuhamasisha matunzo bora ya mama mjamzito, mama anayenyonyesha, na mtoto mchanga kuanzia wakati wa kuzaliwa hadi anapotimiza umri wa miaka miwili.
Ad

Unaweza kuangalia pia

ONGEZENI KASI YA KUWAHUDUMIA WANANCHI – DKT. CHAULA

Watumishi wa afya nchini wametakiwa kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi kwenye vituo vya kutolea huduma …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *