Na Munir Shemweta, DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema Serikali iko katika maandalizi ya kufanya sensa ya nyumba na majengo kote nchini.
Sensa hiyo itafanyika sanjari na Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwezi Oktoba, 2022.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani tarehe 4 Oktoba 2021 jijini Dodoma Lukuvi alisema, Sensa hiyo itasaidia kubaini idadi na hali ya nyumba nchini, hivyo kuiwezesha Serikali na wadau wengine wa maendeleo ya makazi kuchukua hatua muafaka za kuboresha makazi ya watu mijini na vijijini.
‘’Natoa wito kwa wananchi wote kujitokeza katika zoezi la sensa maana hili ni zoezi muhimu sana na kuna uhusiano mkubwa kati ya watu na makazi na lengo hapa ni kujua hali ya makazi nchini na upungufu wake sambamba na kujua vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa nyumba’’ alisema Lukuvi
Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa kila jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba na kauli mbiu ya mwaka huu ni’’Utekelezaji wa haraka wa Majukumu ya kimji ili kuwa na dunia isiyo na Hewa-Ukaa’’ “Accelerating urban action for a caborn free world”
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, kauli Mbiu ya siku ya Makazi Duniani huwezesha kutafakari suala husika kwa kina na kutoa fursa ya kujiwekea nafasi na mazingira wezeshi ya kutafuta ufumbuzi wa muda mfupi, wa kati na muda mrefu wa kukabiliana na suala husika kwa mwaka huo
Katika kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani mwaka huu Waziri Lukuvi alisema, ni vyema kila mwananchi atambue kuwa, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara na taasisi zake imefanya juhudi kubwa katika kupunguza uzalishaji wa hewa-ukaa hususan kwa wakazi wa mijini.
Alitolea mfano wa usambazaji wa nishati ya umeme kwa gharama nafuu mijini na vijijini, uhamasishaji wa matumizi ya gesi ya kupikia majumbani, upigaji marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na kampeni ya kutunza na kuhifadhi misitu na vyanzo vya maji kuwa ni miongoni mwa hatua za kimkakati ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali zikilenga pamoja na mambo mengine kupunguza hewa-ukaa duniani.
Lukuvi alisema Wizara ya Ardhi imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yake makuu matatu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi kwa waendelezaji mbalimbali nchini na kuongeza kuwa, zoezi la Upangaji Matumizi ya Ardhi, Upimaji na Umilikishaji Ardhi nchini, ni utekelezaji ambao pamoja na manufaa mengine ya kiuchumi na kijamii, pia ni hatua ya msingi katika kuzuia uharibifu wa mazingira ya miji na vijiji, unaosababishwa na matumizi ya ardhi yasiyoendelevu na yanayohatarisha usitawi wa Baioanuai.
Alisema kupitia Wizara yake, wataalam wameweza kutoa mchango mkubwa katika kupunguza ongezeko la hewa-ukaa katika miji na majiji kwa Kupanga miji kwa kuheshimu, kutunza na kuhifadhi hali halisi ya kijiografia na kutolea mfano wa vyanzo vya maji; mito/vijito asili; maeneo oevu; mabonde na miinuko pamoja na kuhifadhi misitu ya asili.
Upangaji huo unawezesha ukuaji endelevu wa miji unaowiana na hali halisi ya kiikolojia na ustawi wa baio anuai, Upangaji shikamanifu wa miji (Compact city) unaowezesha ujenzi shadidi (Vertical Development) na hivyo kuepusha msambao wa mji usio na tija (urban sprawl).
‘’Hatua hii inaepusha au kupunguza kasi ya ubadilishaji wa ardhi asili ya kilimo na misitu kuwa mji, Upangaji miji kwa zingatia utengaji toshelevu wa maeneo ya wazi, maeneo ya umma, mitaa mipana ya barabara/njia na mashamba mji, vyote vikishamiri miti ambayo ni mapafu ya mji kwa kuzalisha wingi wa hewa ya oksijeni’’ alisema Waziri Lukuvi.
Aliwasihi wananchi kila mmoja kuitumia siku hii ya Makazi Duniani kutafakari na kuona ni jinsi gani anaweza kuwa balozi mzuri wa kuelimisha na kuhamasisha jamii inayomzunguka ili kuachana na shughuli au vitendo vinavyo huchochea ongezeko la hewa-ukaa nchini na duniani kwa ujumla.
‘’Mtakubaliana nami kuwa, vitendo vya uchafuzi wa mazingira kwa kuzalisha hewa-ukaa, ni suala linalosukumwa zaidi na utashi wa mtu binafsi katika taifa au jamii husika na kuepukana na vitendo hivyo kunahitaji zaidi jamii kuwa na uelewa wa kutosha na pia kuwa na utayari wa kufanya mabadiliko chanya ya kifikra kuliko kuwa na wingi wa rasilimali fedha’’ alisema Lukuvi.