Na Teresia Mhagama, Dodoma
Waziri wa Nishati, January Makamba ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati ipo tayari kufanya kazi na Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS) ili kuendelea kuwezesha wananchi kushiriki ipasavyo katika Sekta hiyo.
Makamba alisema hayo tarehe 4 Oktoba, 2021 wakati alipofanya mazungumzo na Wajumbe wa Bodi hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Abdulsamad Abdulrahim ambapo Jumuiya hiyo ilifika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma kwa kwa ajili ya kueleza malengo yake na masuala mengine yanayohusu Jumuiya hiyo ambayo ina wanachama takriban 128.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, Mkurugenzi Mtendaji wa wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Dkt. James Mataragio na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA), Charles Sangweni.
“Sisi tuko tayari kufanya kazi na ninyi kwani tunaamini wananchi wengi wanaweza kunufaika na fursa zinazotokana na hii sekta kutokana na uwepo wa Jumuiya hii ambayo inawapa wananchi taarifa mbalimbali kuhusu fursa zilizopo pamoja na kuwaunganisha na Mamlaka mbalimbali pamoja na wafanya maamuzi.” Alisema Makamba
Alisisitiza kuwa, Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake zitaunga mkono Taasisi au Jumuiya ambazo zina malengo chanya ikiwemo ya kuwaunganisha wananchi na kuwapa fursa na taarifa zitakazowasaidia katika kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Wajumbe wa Jumuiya hiyo walishukuru uongozi wa Wizara ya Nishati kwa kuwapokea na kuwasikiliza na kueleza kuwa, nia yao ni kushirikiana na Serikali katika utaratibu wowote utakaopelekea wananchi wengi washiriki kwenye shughuli za kiuchumi katika Sekta ya Mafuta na Gesi.