- Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) umepongezwa kwa utekelezaji mzuri wa Sera ya Uchumi wa Viwanda inayohimizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa mikopo kwa makundi maalumu ya watu wenye ulemavu, akina mama na vijana wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali jijini Dar es Salaam.
- Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kuwatembelea watumishi wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea kwa lengo la kufahamu majukumu ya mfuko huo na kuhimiza uwajibikaji, ambapo alipata fursa ya kujionea wanufaika wa mikopo inayotolewa na mfuko huo.
- Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, makundi yaliyopatiwa mikopo ambayo ni kundi maalumu la walemavu la Furaha ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi Tanzania (FUWAVITA), kikundi cha UWAZI SHALOOM cha akina mama wasindikaji, Kikundi cha MAKINI FOOD SUPPLIES cha akina mama wasindikaji na kikundi cha MAB cha vijana ni mfano mzuri wa kuigwa kwa kutekeleza sera ya Uchumi wa viwanda kwa vitendo kwani wanazalisha bidhaa zenye ubora ambazo ni mvinyo, viungo vya mchuzi, viungo vya chai, siagi ya karanga, mango pickle na mabeji ya wanafunzi wa shule za awali, za msingi na vyuo.
- Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, PTF imejitofautisha na taasisi nyingine za kifedha kwani inajali makundi maalumu yote kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na yenye riba ndogo zaidi bila ubaguzi wowote.
- Kwa upande wake, mwakilishi wa kikundi cha Furaha ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi Tanzania (FUWAVITA), Bi. Aneth Gerana amesema wanaishukuru PTF kwa kuwapatia mikopo kwani imekuwa ikiwanufaisha sana ikizingatiwa kwenye mabenki hawadhaminiki hivyo PTF imekuwa mkombozi kwao.
- Bi. Gerana amesisitiza kuwa, kupitia mkopo wa fedha wa PTF wao kama walemavu wameweza kuuthibitishia umma kuwa, wanaweza kwa kuzalisha mvinyo wenye ubora na kuongeza kuwa wana hakika ya kuifikia ndoto ya kuwa na kiwanda cha mvinyo kikubwa Afrika ya Mashariki ili kuunga mkono kwa vitendo sera ya uchumi wa viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano.
- Bi. Gerana, ameiomba PTF kuwapatia mafunzo ya kompyuta wao kama kundi maalumu la walemavu ili mafunzo hayo yaweze kuwasaidia kutafuta masoko kwa njia ya mtandao, ombi ambalo lilitiliwa mkazo na Mhe. Dkt. Mwanjelwa kwa kuitaka PTF kuwapatia mikopo ya vifaa itakayowawezesha kununua kompyuta zitakazowarahisishia utafutaji wa masoko kwa njia ya mtandao.
- Naye, Mwakilishi wa kikundi cha MAB cha vijana wanaotengeneza mabegi, Bw. Amon Philemon amesema mkopo wa PTF umewawezesha kuwa wajasiriamali wa kutengeneza mabegi ya wanafunzi wa kuanzia shule za awali hadi vyuo vya elimu ya juu.
- Bw. Philemon ameainisha kuwa, katika mabegi wanayoyatengeneza wanaweka picha za wanafunzi husika, majina yao na logo, lengo likiwa ni kudhibiti wizi mashuleni na vyuoni, hivyo Dkt. Mwanjelwa amekipongeza kikundi hicho kwa ubunifu huo.
- Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) ni Taasisi ya Kifedha inayotoa mikopo ya fedha na vifaa nchini kwa makundi ya akina mama wajasiriamali wazalishaji, kundi maalumu la watu wenye ulemavu na vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi lengwa kabla ya kutoa mikopo kwa wanufaika hao wa PTF.
Ad
Mfuko was rais mkoa wamorogoro ulitukomboa sn sisi akina mama wajane ,tangu nilipojiunga nilipata mafanikio makubwa nawazo yaliisha kwani niliamini nipo kwenye chombo salama,lkn walipokuja akina dastani wakatuvuluga mkasitisha uduma,baadae uduma zikaanza Tena kwa ishawishi mkubwa tukajiunga Tena,Sasa chakusikitisha nikwamba toka tr 23-1-2019,tumemaliza mikopo Lkn hakuna uduma Tena,akina zetu hatupewi tukipiga sima tukauliza tunaambiwa tatizo liko makao makuu,Sasa ndio uduma Bora tunazopata kweli maana ata uzalishaji uyoga tumesidha mashamba yamekufa,hatujui hatma zetu,bc tupewe viakiba vyetu tujue Nini tufanye,mh mwenye dhama na kilio iki kikufikie najua unatujali akina mama wenzio,tunaangamia.
Asante kwa Taarifa