RAIS MAGUFULI AKUTANA NA RAIS MSTAAFU WA NIGERIA

  • Rais  Dkt. John Magufuli leo tamekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Dkt. Olusegun Obasanjo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
  • Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Obasanjo amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika uongozi wake ikiwemo kupambana na rushwa, kuimarisha utoaji wa elimu, kuimarisha miundombinu, kuongeza nishati ya umeme, kuboresha usafiri wa ardhini na angani na jinsi wadau mbalimbali wa ndani na nje wanavyopaswa kuelewa juhudi zinazofanyika.
OBA-1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
  • Mhe. Dkt. Obasanjo amesema Mhe. Rais Magufuli amedhihirisha kuwa kiongozi imara wa kusimamia mambo muhimu yenye maslahi kwa nchi yake na amebainisha kuwa licha ya kwamba maendeleo ya nchi hayapatikani mara moja lakini kwa muda mfupi Mhe. Rais Magufuli amefanya juhudi kubwa za kuimarisha maeneo ya huduma za kijamii, kukiimarisha chama chake cha siasa (Chama Cha Mapinduzi – CCM) na kwamba ameonesha kuwa anakijua anachokifanya katika maeneo ya uchumi.
  • “Tusijisahau kwamba ukoloni mamboleo bado upo na mabeberu bado wanaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha wanatunyonya, na kiongozi yeyote wa Afrika anayethubutu kuwazui hawezi kuwa rafiki wa hao ambao walikuwa wakinufaika kwa kutunyonya” amesisitiza Mhe. Dkt. Obasanjo.
  • Mapema kabla ya kukutana na Mhe. Dkt. Obasanjo, Mhe. Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho za Mabalozi watatu walioteuliwa kuziwakilisha nchi za Jamhuri ya Korea, Malawi na Brazil hapa nchini, baada ya waliokuwa Mabalozi wa nchi hizo kumaliza muda wao.
  • Waliowasilisha hati hizo ni Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Mhe. Cho Tae-ics aliyechukua nafasi ya Mhe. Song Geum-young,  Balozi wa Malawi hapa nchini Mhe. Glad Chembe Munthali aliyechukua nafasi ya Mhe. Hawa Olga Ndilowe na Balozi wa Brazil hapa nchini Mhe. Antonio Augusto Martins Cesar aliyechukua nafasi ya Mhe. Carlos Alfonso Iglesias Puente.
  • Mabalozi wote wamemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa katika kipindi chao watakahakikisha wanaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo na matunda ya uhusiano na ushirikiano huo yanawanufaisha wananchi wa pande zote.
  • Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Cho Tae-ics kwa kuteuliwa kuiwakilisha Jamhuri ya Korea hapa nchini na amemtaka apelekee salamu zake za shukrani kwa Rais wa Korea Mhe. Moon Jae-in kwa ushirikiano mzuri ambao Tanzania inaupata kutoka Korea ikiwemo kujengwa kwa miundombinu kama vile Daraja la Kikwete lililopo mto Malagarasi Mkoani Kigoma, Hospitali ya Mafunzo na Tiba Mloganzila na Daraja la Tanzanite linalounganisha ufukwe wa Aga Khan na Coco Beach Jijini Dar es Salaam, na pia amemuomba kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya Makao Makuu Jijini Dodoma ili kuweka alama ya ushirikiano kati ya Tanzania na Korea.
  • Kwa Mhe. Glad Chembe Munthali, Mhe. Rais Magufuli amemuomba afikishe salamu zake kwa Rais wa Malawi Mhe. Prof. Arthur Peter Muthalika na kumhakikishia kuwa Tanzania itadumisha na kukuza zaidi uhusiano wa kirafiki na kidugu uliopo kati yake na Malawi na kwamba endapo Malawi itahitaji kununua chakula, Tanzania ipo tayari wakati wowote kutoa chakula hicho.
  • Mhe. Rais Magufuli amemtaka Balozi wa Brazil hapa nchini Mhe. Antonio Augusto Martins Cesar kufikisha salamu zake kwa Rais wa Brazil Mhe. Jair Bolsonaro na kumshukuru kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Brazil na Tanzania na pia ameiomba nchi hiyo ishiriki katika uzalishaji wa nishati ya umeme kwa ajili ya kuendeleza viwanda hapa nchini ikiwemo kuwekeza katika mradi wa kuzalisha umeme katika mto Luhuji Mkoani Njombe wenye uwezo wa kuzalisha Megawatts kati ya 350 na 400.

 

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: UZINDUZI WA MAJENGO YA OFISI YA MANISPAA NA MKUU WA WILAYA KIGAMBONI JIJINI DSM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11, Febuari, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *