- NAIBU Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa ameagiza Wakala wa Majengo Nchini (TBA) kuhakikisha wanamaliza Mradi wa Nyumba za Kisasa wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam unamalizika kufikia mwezi Desemba mwaka huu.
- Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Kwandikwa ametoa msisitizo huo leo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara kukagua maendeleo ya mradi huo.
- Amesema kuanzia sasa atakuwa akiutembelea mradi huo kila mwezi ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa na hatimaye mradi ukamilike Desemba kama ilivyoagizwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli alipoutembelea mradi huo hivi karibuni.
- “…Kuanzia leo nitahakikisha nawatembelea hapa kama sio kila wiki basi kila mwezi, lengo langu ni kuhakikisha mradi huu mkubwa unakamilika kwa wakati na wananchi hawa wapatao 656 waliokuwa wakiishi hapa wanaingia na kuanza kuzitumia nyumba hizi,” alisema Naibu Waziri.
- Aidha aliongeza kuwa wizara yake itahakikisha inafika eneo hilo kila mara kutatua changamoto zote ambazo zitakuwa zikihitaji kutatuliwa na wizara hiyo, huku akionya itakuwa ni jambo la kushangaza endapo mradi huo utasimama tena na kumlazimu Rais Dk. Magufuli arudi tena eneo hilo.
- “…Sisi kama wizara tunataka endapo Mh. Rais Dk. John Pombe Magufuli akija tena eneo la Magomeni Kota ni kufanya uzinduzi wa nyumba zikiwa zimekamilika na si vinginevyo,” alisisitiza Naibu Waziri Kwandikwa akizungumza na viongozi na waandisi wa TBA wanaosimamia mradi huo.
- Aliipongeza TBA kwa kitendo cha kuanza kutumia mitambo ya kisasa ya kufyatua matofali, kuchanganya na kubeba zege hadi gorofani jambo ambalo litaongeza kasi ya ujenzi na ufanisi katika mradi huo.
- Aliwataka kuangalia namna ya kuanza haraka kufanya kazi usiku na mchana kutokana na ujio wa mitambo hiyo. Alisema wazo la kuanza kufanya kazi usiku na mchana licha ya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi linatoa fursa kwa vijana wengi sasa kuja kufanya kazi na kujipatia kipato.
- Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA, Eng. Jasper Lugemarila akizungumzia changamoto zilizokwamisha mradi huo awali, alisema ilikuwa ni kupanda kwa bei ya zege ambayo walikuwa wakinunua pamoja na bidhaa nyingine kama simenti, kokoto na nondo.
- Alisema kwa sasa wamekwisha tatua changamoto hizo baadha ya kuanza kutengeneza zege wenyewe kwa kutumia mitambo ya kisasa inayoendeshwa na kompyuta.
- “…Mwanzoni tulikuwa tunamimina zege kwa kununua kutoka kwa wafanyabiashara hiyo, lakini walipoona mradi huu umeanza na ni mkubwa wakatupandishia bei sana wakijua lazima twende kwao,” alisema Eng. Jasper Lugemarila
Ad