SHIRIKISHO LA JAMHURI YA UJERUMANI LIMETOA MSAADA WA EURO MIL 8 KUBORESHA TEKNOLOJIA YA TEHAMA KATIKA MFUKO WA BIMA WA NHIF

  • Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani limetoa msaada wa Euro milioni 8 ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 20 kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwaajili ya kuboresha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mfuko wa Bima ya Afya nchini NHIF.
  • Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini wa msaada huo, Kaimu Balozi wa Ujerumani nchini Bw.Jorg Herrera amesema msaada huo ni kwaajili ya kuimarisha mfuko wa Bima ya Afya ili uweze kuwahudumia watanzania wengi zaidi hasa wale wa vijijini.
11-01
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na akimpa mkono wa shukurani Kaimu Balozi Bw. Jorg Herrera mara baada ya kutia saini mikataba hiyo,hafla hiyo fupi ilifanyika jana katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.
  • Amesema lengo la Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani ni kuisaidia Serikali ya Tanzania katika azma yake ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama wa mfuko wa Bima ya Afya ili hatimaye kufikia lengo la kutoa huduma ya Afya kwa wote .
  • Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw.Doto James amesema msaada huo umekuja wakati muafaka ambapo Serikali ya Awamu ya Tano inajitahidi kuboresha huduma za Afya kwa wananchi wake ili waweze kufanya kazi kwaajili ya kuelekea Tanzania ya Viwanda.
  • “Msaada huu ni wa masharti nafuu kabisa na hatulazimiki kulipa fedha yoyote, na sisi kama Serikali tumeupitia na kujiridhisha kwamba hauna chembe yoyote ya masharti ndio maana leo hii tumetoka hadharani kusaini ” Alisema.
22-01
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Kaimu Balozi Bw. Jorg Herrera Wakionesha nakala za Mikataba ya Msaada baada ya kutia saini .Hafla hiyo fupi ilifanyika jana katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.
  • Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha alisema msaada wowote ambao serikali inapatiwa hupitiwa na wataalam makini ambao wanahakikisha hakuna masharti ambayo yatakuja kusumbua baadaye na pia ni kwa kuzingatia Sheria na Katiba ya nchi.Pia amesema kwa upande wa Ujerumani wamekuwa marafiki wazuri sana ambao mara kwa mara wameendelea kuisidia Serikali katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
  • Aidha Bw. James amesema uimarishaji wa mfumo wa TEHAMA katika mfuko wa Bima ya Afya una manufaa makubwa ikiwemo,kuongeza usajili wa wanachama wa bima ya Afya ikiwajumuisha walioko kwenye sekta isiyo rasmi pia kuboresha namna ya kuwatambua ,kuwasajili na kuwalipa watoa huduma.
  • Faida nyingine ni kuboresha utendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake za kila siku pamoja na kuwajengea uwezo wa watumishi wa mfuko wa Bima ya Afya.
33-01
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James akisaini Mkataba wa Msaada wa Shilingi Bilioni 20 Kati yake na Kaimu Balozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Bw.Jorg Herrera, Hafla hiyo fupi ilifanyika jana katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.
  • Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeazimia kutoa huduma za Afya kwa wote na ili kufikia lengo hili, kuna mpango wa kuwa na mfuko mmoja wa Bima ya Afya utakaojulikana kama “Single Health Insurance Fund” (SNHIF) ambapo itakuwa ni lazima kila mtanzania kujiunga.
  • Serikali ya ujerumani siyo mara ya kwanza kuisaidia Tanzania, kwani imekuwa ikisaidia katika sekta za Maji, Nishati,Uhifadhi wa maliasili,Usimamizi wa fedha za umma pamoja na kuijengea uwezo Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
  • Hivi karibuni Serikali ya Tanzania imeshuhudia mashirika ya kimataifa nchi mbalimbali pamoja na wahisani wakiendelea kumimina misaada kwaajili ya shughuli za maendeleo kutokana na uongozi wa Rais Dkt.John Magufuli , ambao umejitahidi kupambana na ufisadi na kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wengi. Na.Mwandishi Wetu –MAELEZO
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI UMMY AWATAKA WAZAZI KUWEKEZA KATIKA AFYA ZA WATOTO

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewataka wazazi kuwekeza …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *