- Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa kuokoa kiasi cha shilingi Bilioni 10.08 kutokana na kaguzi za gharama na mapato ya mikataba ya Mafuta na Gesi Asilia nchini (PSAs).
- Pongezi hizo wamezitoa tarehe 25 Oktoba, 2019 wakati wa kikao baina ya Kamati hiyo na Wizara ya Nishati pamoja na PURA ambapo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliiongoza Wizara ya Nishati katika uwasilishaji wa taarifa hiyo akiwa ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hamisi Mwinyimvua na Menejimenti ya Wizara, PURA na Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara.
- Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni alisema kuwa kama kaguzi hizo zisingefanyika, wawekezaji wangeweza kujirudishia fedha hizo (cost recovery) kulingana na mkataba hivyo kiasi hicho kilichookolewa kitafanya mapato ya Serikali kuongezeka wakati wa ugawanaji wa faida itokanayo na mauzo ya Gesi Asilia.
- “ PURA ilianza kutekeleza jukumu hili kwa kufanya kaguzi za gharama na mapato kuanzia mwaka 2016 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 10.08 zimeokolewa hadi sasa.” Alisema Sangweni
- Sangweni alieleza kuwa Mamlaka hiyo pia imeendelea kufanya kaguzi katika maeneo ya uzalishaji wa Gesi Asilia kwa lengo la kuhakiki usalama wa mazingira na wafanyakazi pamoja na kupata uhalisia wa shughuli zinazotekelezwa katika uzalishaji wa Gesi Asilia nchini.
- Alisema kuwa, katika kipindi cha robo mwaka wa 2019/2020, masuala mbalimbali yaliangaliwa na kuhakikiwa na kaguzi hizo zilibaini kuongezeka kwa uzalishaji wa Gesi Asilia ambapo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2018/19 uzalishaji ulikuwa ni futi za ujazo bilioni 15.73 na kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2019/20 uzalishaji ulikuwa ni futi za ujazo bilioni 16.05.
- Alisema kuwa, kwa ujumla Gesi iliyogunduliwa nchini hadi sasa ni takriban futi za ujazo Trilioni 57.54 ambapo kati ya kiasi hicho, Gesi iliyogunduliwa nchi kavu (onshore) ni futi za ujazo Trilioni 10.41 na kwa upande wa Bahari Kuu (offshore) ni futi za ujazo Trilioni 47.13.
- Aidha alisema kuwa, kaguzi za PURA zilibaini kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi wazawa katika kampuni zinazozalisha Gesi Asilia huku akitolea mfano kampuni ya PanAfrican Energy na Maurel et Prom ambapo idadi ya wafanyakazi wazawa imefikia zaidi ya asilimia 90.
- Sangweni pia aliieleza Kamati ya Bunge kuhusu kazi inayofanywa na Mamlaka hiyo katika kusimamia shughuli za utafutaji na uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ya kusimamia shughuli ya uchukuaji wa data na uchorongaji katika Kitalu cha Eyasi Wembere kilicho chini ya TPDC ambapo visima vifupi vitatu vya utafiti wa awali vimeanza kuchorongwa.
- Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alieleza kuhusu faida mbalimbali za uwepo wa Gesi Asilia nchini ikiwemo kuwa kama chanzo cha kuzalisha umeme nchini kwani zaidi ya asilimia 57 ya umeme unaozalishwa unatokana na Gesi Asilia.
- Aidha alieleza kuhusu juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa PURA inatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuongeza bajeti ya Taasisi hiyo, kukamilisha muundo wa Taasisi hiyo na kuipatia fedha kwa wakati.
Ad
Kazi nzuri, changamoto nyingi zipo kwenye offshore pia, so muendelee kufanya cost auditing, ili Taifa linufaike Zaid na non renewable resources zake.