WANANCHI WENGI WAJITOKEZA KUFANYIWA UCHUNGUZI SARATANI YA MATITI

  • Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania-MEWATA- imefanya zoezi la uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti bila malipo kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya ugonjwa huo na kuhamasisha jamii umuhimu wa kujichunguza mapema. 
  • Zoezi la uchunguzi limefanyika kwa siku mbili ambapo kina mama zaidi ya 200 wamehudumiwa huku 45 wakigundulika kuwa na viashiria vya saratani ya matiti hivyo wanahitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi.
3-01
Muwakilishi kutoka MEWATA mkoa wa Pwani Dkt. Deograsia Mkapa akitoa elimu kwa kina mama kuhusu ugonjwa wa saratani ya matiti, ambapo zaidi ya kina mama 200 wamejitokeza kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa awali katika Hospitali ya Mloganzila kati ya hao 45 wamekutwa na viashiria.
  • Daktari Bingwa wa Radiolojia kutoka MNH-Mloganzila Dkt. Lulu Sakafu ametaja huduma zilizotolewa kuwa ni elimu ya ugonjwa wa saratani ya matiti, dalili zake na jinsi ya kujichunguza mwenyewe.
  • “Kujichunguza ni muhimu hasa kwa kina mama ambao ndio waathirika wakubwa wa saratani ya matiti kutokana na uwepo wa vichocheo (Hormone) katika miili yao ambavyo vinaweza kuchangia kupata ugonjwa huu’’ amesema Dkt. Sakafu.
4-01
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili- Mloganzila, Dkt Julieth Magandi akiwa katika picha ya pamoja na watoa huduma mara baada ya kumalizika kwa zoezi la uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti lililofanyika kwa siku mbili.
  • Kwa upande wake muwakilishi kutoka MEWATA ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani Dkt. Sikudhani Muya, amesema tatizo la saratani ya matiti ni kubwa na huathiri wanawake kati ya umri wa miaka 28 hadi 50 kwa asilimia kubwa, na ni asilimia moja tu ya wanaume hukutwa na ugonjwa huu.
2-01
Mtaalam wa mionzi, mawimbi sauti na usumaku wa Hospitali ya Mloganzila Mariam Ndosa (kulia) akichukua vipimo vya urefu na uzito kabla ya Bi. Masha Jum kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti.
  • “Uchunguzi kama huu husaidia kugundua iwapo mtu anaviashiria vya saratani ya matiti na kisha hufanyiwa uchunguzi wa kina na kupelekwa kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya saratani kwa hatua zaidi” amefafanua Dkt. Muya.
  • Saratani ya matiti ni ya pili katika saratani zinazowapata wakina mama hapa nchini ya kwanza ikiwa ni saratani ya shingo ya kizazi.
Ad

Unaweza kuangalia pia

ONGEZENI KASI YA KUWAHUDUMIA WANANCHI – DKT. CHAULA

Watumishi wa afya nchini wametakiwa kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi kwenye vituo vya kutolea huduma …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *