TUNA VIFAA VYA UMEME VINGI VYA KUTOSHA – DKT KALEMANI

 • Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewataka Mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika mikoa yote, kutowaambia wananchi kuwa kuna uhaba wa vifaa vya kuunganishia umeme kwani vilivyopo idadi yake ni kubwa kuliko matumizi ya nchi.
 • Aliyasema hayo wakati akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, akiwa katika ziara ya kazi Desemba 10, 2019.
 • Akifafanua, Dkt Kalemani alisema baadhi ya watendaji wa shirika hilo hawatoi huduma ipasavyo kwa wateja, wakitumia kisingizio kuwa hawana vifaa husika zikiwemo nguzo, nyaya, transfoma na na mita za luku, suala ambalo siyo kweli.
 • “Meneja yeyote atakayeshindwa kumuunganishia mwananchi umeme kwa kisingizio cha ukosefu wa vifaa, hatutamwelewa,” alisisitiza Waziri.
 • Akitoa takwimu ya vifaa husika, Waziri alisema kwa sasa, nchi ina viwanda tisa ambavyo vinazalisha nguzo zaidi ya milioni mbili kwa mwaka wakati mahitaji ni milioni 1.2.
 • Vilevile, alisema mahitaji ya transfoma kwa nchi ni chini ya 210,000 wakati zinazozalishwa ni zaidi ya idadi hiyo kwa mwaka na kwamba nchi ina viwanda zaidi ya vinne vya kuzalisha transfoma.
1-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma kueleza dhamira ya ziara yake wilayani humo, Desemba 10, 2019. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Sophia Kizigo na kushoto kwa Waziri ni Mbunge wa Namtumbo, Mhandisi Edwin Ngonyani.
 • Kwa upande wa mita za luku, alisema vipo viwanda vitatu vikubwa vinavyozalisha mita zaidi zaidi ya milioni mbili wakati mahitaji ni 1,490,000 kwa mwaka.
 • “Awali, tulikuwa na changamoto ya nyaya maana kulikuwa na kiwanda kimoja tu. Sasa hivi tuna viwanda vitano vinavyozalisha zaidi ya kilomita laki tano wakati mahitaji yetu ni chini ya laki 2.5 kwa mwaka.
 • Katika hatua nyingine, Waziri alisema hali ya upatikanaji umeme kwa mkoa wa Ruvuma ni nzuri na kwamba zipo changamoto chache ambazo serikali inazifanyia kazi.
 • Alisema, moja ya mikakati mikubwa inayotekelezwa ni kuunganisha kwenye gridi ya Taifa baadhi ya vijiji vya Namtumbo hadi Tunduru vilikuwa havijaungwa ili viwe na umeme wa uhakika.
 • Waziri aliieleza Kamati ya Ulinzi na Usalama kuwa, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika Desemba 12 na kwamba ifikapo Desemba 13, 2019, gridi ya Taifa kutoka Songea – Namtumbo – Tunduru itawashwa na kuzima mashine inayotumia mafuta mazito iliyopo Tunduru.
 • Katika ziara hiyo, Waziri aliwasha umeme katika kijiji cha Mwangaza wilayani humo ambapo aliwasisitiza watendaji wa TANESCO kuwahamasisha wananchi wengi wajitokeze kulipia shilingi elfu 27 ili waunganishiwe umeme.
 • Alifuatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Sophia Kizigo na Mbunge wa jimbo hilo Mhandisi Edwin Ngonyani. Viongozi hao kwa nyakati tofauti, waliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa namna inavyopambana kuhakikisha wananchi wa vijijini wanafikiwa na huduma ya umeme.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *