ACHENI KULALAMIKA, TENGENI FEDHA KULIPIA UMEME – DKT KALEMANI

  • Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewataka baadhi ya wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri za wilaya ambao wamekuwa wakilalamika kuwa taasisi za umma katika maeneo yao hazina umeme, waachane na malalamiko, badala yake watenge fedha za kulipia huduma hiyo ili wapatiwe umeme.
2-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) akiwa amefuatana na mwenyeji wake, Mbunge wa Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, baada ya kuwasha rasmi umeme katika jengo la Kituo cha Afya cha Kihagala wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma, Desemba 11, 2019
  • Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti Desemba 11, 2019 akiwa katika ziara ya kazi wilayani Nyasa na Songea, mkoani Ruvuma.
  • Dkt Kalemani alieleza kuwa, uzoefu alioupata katika ziara zake sehemu mbalimbali nchini unaonesha kuwa sababu ya taasisi nyingi za umma kutounganishiwa umeme ni viongozi wake kutolipia huduma hiyo.
3-01
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba (kushoto), akimweleza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia) na Ujumbe wake, hali ya upatikanaji umeme wilayani humo, wakati wa ziara yake kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi, Desemba 11, 2019
  • Alisema, wengi wamekuwa wakilalamika, lakini serikali inapofuatilia inagundua kuwa taasisi husika hazijalipia huduma hiyo.
  • “Wengi wao wanatenga fedha za ujenzi wa taasisi lakini wanasahau kutenga bajeti ya umeme halafu wanalalamika.”
4-01
Mbunge wa Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na wananchi (hawapo pichani) wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa kwanza-kushoto) alipofika kijiji cha Kihagala wilayani Nyasa, kuwasha rasmi umeme, Desemba 11, 2019
  • Akitoa hamasa zaidi kwa viongozi hao kutekeleza maelekezo yake, Dkt Kalemani aliwataka watumie fursa iliyotolewa na serikali vijijini, ambapo gharama za uunganishaji umeme zimeshushwa.
5-01
Zoezi la kuunganisha umeme likiendelea katika kijiji cha Kihagala wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma. Taswira hii ilinaswa Desemba 11, 2019 wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipofika kijijini hapo kuwasha rasmi umeme.
  • “Hata taasisi zitakazounganishwa kwa mfumo wa njia tatu (three phase), bado gharama yake ni ndogo sana ukilinganisha na inayotozwa mjini. Badala ya kulipia mamilioni, utalipia laki na sehemu tu hivyo changamkeni.”
  • Katika ziara hiyo, Waziri aliwasha umeme katika vijiji vya Liuli na Kihagala vilivyoko wilayani Nyasa pamoja na vijiji vya Liganga na Nguvumoja vilivyoko wilaya ya Songea.
6-01
Sehemu ya majengo ya Kituo cha Afya cha Kihagala wilayani Nyasa. Hospitali hii iliwashiwa rasmi umeme na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), Desemba 11, 2019.
  • Aidha, pamoja na mambo mengine, alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma na miradi mbalimbali ya maendeleo kupewa kipaumbele katika kuunganisha umeme ili ziweze kuwahudumia vema wananchi.
7-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Liuli wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma, alipofika kuwawashia rasmi umeme, Desemba 11, 2019.
  • Waziri aliwapongeza viongozi wa maeneo hayo wakiwemo wabunge Stella Manyanya (Nyasa) na Jenista Mhagama (Peramiho) pamoja na Wakuu wa Wilaya husika, Madiwani na wengine ngazi ya halmashauri na vijiji, kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme bila kuchoka ili kuhakikisha wananchi wao wanafikiwa na nishati hiyo.
8-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili-kushoto), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Kanisa la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Parokia ya Liganga, wilayani Songea, Desemba 11, 2019.
  • Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi hao, akiwemo Mbunge wa Nyasa Mhandisi Manyanya pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, Isabela Chilumba, wameipongeza Serikali kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, hususan walioko vijijini.Veronica Simba – Ruvuma
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *