MADAKTARI KUTOKA NCHINI CHINA WANAOFANYA KAZI NCHINI WATOA MSAADA WA VIFAA TIBA NA DAWA ZENYE THAMANI YA SH. 15 MILIONI KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI)

  • Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetumia zaidi ya  shilingi bilioni 1.2 kwa mwaka 2019 kwa ajili ya kulipa gharama za matibabu ya moyo kwa wagonjwa wanaotoka katika familia maskini na  wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama hizo.
  • Hayo yamesemwa  na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Agnes Kuhenga wakati akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya  kupokea msaada wa vifaa tiba pamoja na dawa kutoka Ubalozi wa China kupitia Timu ya madaktari kutoka nchini humo wanaofanya   kazi hapa nchini.
  • Agnes ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utawala na Fedha alisema asilimia 10 hadi 15 ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo hawana kadi za bima ya afya na hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu. Wagonjwa wa aina hiyo wanapata huduma za matibabu kwa Taasisi   kugharamia matibabu yao.
1-01
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kuhenga pamoja na kiongozi wa timu ya madaktari kutoka Jamhuri ya watu wa China wanaofanya kazi hapa nchini Dkt. Quin Chengwei wakiweka saini makubaliano ya makabidhiano ya dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 15 zilizotolewa na Ubalozi wa China kupitia madaktari hao kwa ajili ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu wanaotibiwa katika Taasisi hiyo. Hafla fupi ya makabidhiano hayo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
  • “Januari mwaka huu hadi siku hii ya  tarehe 19/12/2019  tumetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa ambao hawakuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu. Ninaiomba mifuko ya bima za afya iweze kutoa elimu kwa watanzania  ili wajiunge na bima hizo ambazo zitawapunguzia wananchi gharama ya kulipia fedha za matibabu pindi watakapougua”, alisema Agnes.
  • Akizungumzia kuhusu  msaada huo Agnes aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa misaada mbalimbali ya huduma za afya wanayoitoa katika Taasisi hiyo na kwa upande wa vifaa tiba pamoja na dawa walizozitoa alisema zitatumika kwa wagonjwa  wasiokuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu.
  • Kwa upande wake mwakilishi wa Balozi wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini Yuan Lin alisema msaada wa vifaa tiba pamoja na dawa walizozitoa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia madaktari wa Kichina wanaofanya kazi hapa nchini unathamani ya shilingi milioni 15.
  • “Ninaamini msaada huu ambao ni moja ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya afya utasaidia katika matumizi ya kila siku ya Hospitali na utachangia katika kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa”, alisema Lin.
Ad

Unaweza kuangalia pia

ONGEZENI KASI YA KUWAHUDUMIA WANANCHI – DKT. CHAULA

Watumishi wa afya nchini wametakiwa kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi kwenye vituo vya kutolea huduma …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *